Na. Judith Damas
Uongozi wa Kata ya Kipunguni kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya Maendeleo ya Jamii leo Januari 27, 2022 wameeandaa tamasha la maonyesho ya wajasiriamali wa Kata ya Kipunguni yaliyofanyika katika viwanja vya Moshi Bar Kata ya Kipunguni Jijini Dar es salaam lengo likiwa ni kutambulisha bidhaa zao na kutoa elimu kwa wajasiriamali wanaofanya biashara na wanaotaka kuanzisha biashara zao ambapo ni utekelezaji wa Sera ya Taifa ya uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004.
Akiongea katika tamasha hilo mgeni rasmi ambaye ni Naibu Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Saady Khimji amesema "Kwa niaba ya Mstahiki Meya Pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam napenda kuwahakikishia wananchi wajasiriamali wa Kata ya Kipunguni Kuwa tutashirikiana nanyi ili kuweza Kuwawezesha wananchi wetu kujikwamua kiuchumi hususani wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha Mhe. Khimji amewapongeza Wajasiriamali wa Kata ya Kipunguni kwa kazi nzuri wanazozifanya hivyo amewaomba wajasiriamali waliopata mkopo waweze kurudisha kwa wakati ili kuwapatia fursa wajasiriamali wengine kupata mkopo na kuendesha biashara zao.
Akitoa taarifa fupi ya vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu Afisa maendeleo wa Kata ya Kipunguni Bi. Rozina Soka ameeleza kuwa Kata ya Kipunguni ni miongoni mwa Kata 36 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambazo zimenufaika na mikopo ya asilimia 10% za mapato ya ndani inayolenga kuwawezesha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kuanzia mwaka 2019 hadi kufikia mwaka 2021.
Aidha Bi.Rozina ameendelea kusema hadi kufikia Disemba 2021 Kata ya Kipunguni imeweza kusajili vikundi 46 ambavyo vimepokea mkopo wa shillingi milioni 432.5 ambapo vikundi thelathink (30) vya wanawake wamepokea shilingi milioni 217 huku vikundi kumi na nne (14) vya vijana vimepokea shilingi milioni 159.5 na vikundi viwili (2) vya watu wenye ulemavu vimepokea jumla ya shilingi milioni 56.
Sambamba na hilo Bi Rozina Soka amesema " Tunaishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kupitia Idara ya maendeleo ya jamii kwa kutuwezesha kupata mikopo japo kuna changamoto katika ufuatiliaji wa marejesho lakini sisi kama viongozi tumeandaa mikakati ya ufuatiliaji ngazi ya kata lengo likiwa ni kuhakikisha fedha zote za mkopo zinarejeshwa kwa wakati na vikundi vingine vinavyoomba mikopo viweze kupatiwa kwa wakati.
Vilevile shillingi milioni 598 inatarajiwa kutolewa kwa vikundi takribani arobaini na moja(41) ambavyo vishajadiliwa kwenye kikao cha kamati ya fedha na mara tu watakapokamilisha taratibu zilizobaki watapatiwa mkopo huo.
Akitoa wito kwa wananchi kwa niaba ya wajasiriamali wenzake wa Kata ya Kipunguni Bi. Mboni Edd Gamuya amesema "Napenda kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuona tija ya kutupatia mkopo kwani mikopo hii imeweza kutukwamua kiuchumi na pia kwa kiasi kikubwa imeweza kutatua tatizo la ajira kwa vijana wengi.Pia ningependa kutoa wito kwawajasiriamali wenzangu ambao wanasuasua kurejesha mikopo yao warejeshe kwa wakati ili kuwapatia fursa wananchi wengine wanaoomba mikopo waweze kupata mikopo kwa wakati na kuweza kuendesha biashara zao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.