Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija, amewaagiza wenyeviti na watendaji wa mitaa katika Wilaya ya Ilala kushughulikia changamoto za urasimishaji ardhi katika maeneo ya kufuatia malalamiko ya wananchi dhidi ya makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji ardhi kwa niaba ya Serikali.
“Nahitaji makampuni yote binafsi kusimamia urasimishaji wa ardhi kwa kushirikiana na kamati zilizoundwa na Serikali za Mitaa kuhakikisha jukumu la urasimishaji ardhi linakuwa na matokeo chanya ambayo yatatutoa katika changamoto za migogoro ya kila siku,” amesema Ludigija.
Mkuu huyo wa Wilaya amewaeelekeza watendaji wake kuendelea kutoa elimu ya ya kutosha kwa wananchi kuhusu urasimishaji wa ardhi na faida zitokanazo na zoezi hili ili wananchi wawe na mwamko wa kuchangia kiasi cha fedha kilichopangwa na serikali.
“Ombi langu kwa wenyeviti wote wa mitaa na watendaji wote ni kufanya vikao na wananchi wenu na kutoa elimu juu ya umuhimu wa urasimishaji ardhi kwa kutambua kwamba zoezi hili ni la kitaifa na kila mwananchi anapaswa kurasimisha sehemu yake,” amesema Ludigija.
Mhe. Ludigija amewaeleza watendaji hao kuwa zoezi hilo litasaidia kuimarisha usalama, kutoa fursa kwa wamiliki wa ardhi kupata na kunufaika na mikopo kutoka katika benki mbalimbali nchini. Aidha, ameyataka makampuni yote ya urasimishaji kuhakikisha wanakutana na kujadiliana kuhusu changamoto zinazosababisha baahi ya kampuni kushindwa kufanya kazi zao na kupotea na fedha za wanachi.
Kupitia fursa ya mkutano huo wa Mkuu wa Wilaya ambao ulihudhuriwa na wenyeviti na watendaji wa Serikali za Mitaa, wawakilishi wa makampuni ya urasimishaji ardhi na wadau mbalimbali katika sekta ya ardhi, mwakilisha wa Benki ya NMB, Irene Masaki ambaye ni Meneja Uhusiano kutoka katika kitengo cha huduma kwa wateja Kanda ya Dar es Salaam inayohusisha mikoa ya Pwani na Morogoro amesema kuwa benki ya NMB inafungua milango ya mikopo kwa wananchi kuwawezesha kupata fedha za kuchangia katika zoezi la urasimishaji.
Masaki amesema kuwa benki hiyo itatoa mikopo ya fedha kuanzia kiasi cha shilingi laki mbili hadi milioni moja ambacho taratibu zake za urejesha zina masharti nafuu ya kuwawezesha wananchi kurejesha kiasi kidogo cha fedha katika kipindi cha mwaka mmoja ili kuhakikisha suala hili la urasimishaji linafikia malengo.
Akiongea kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Tabu Shaibu, amesema Halmashauri ya Jiji itasimamia zoezi hilo katika kila kata kuweza kufikia malengo ya Serikali juu ya urasimishaji wa ardhi nchini..
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.