Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 12 Oktoba, 2020 imepokea ugeni wa maafisa wa kijeshi kutoka Chuo cha Ukamanda na Unadhimu kilichopo eneo la Duluti nje kidogo ya Jiji la Arusha kwa ajili ya ziara ya mafunzo.
Ujumbe huo wa Maafisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na majeshi mengine ya Ulinzi kutoka nchi za Afrika ukiongozwa na Brigedia Generali S.D. Ghuliku umetembelea ofisi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kupokelewa na mwenyeji wao Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam John Masero.
Maafisa hao wanaochukua mafunzo ya Ukamanda na Unadhimu wa Jeshi walifanya mazungumzo na Mkurugenzi Masero pamoja na wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo ya mafunzo, ujumbe huo uliokuwa na maafisa wasiopungua 50 ulitaka kujifunza katika maeneo yafuatayo:
•Uongozi na Utawala wa Sheria
•Majukumu/Shughuli kuu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
•Ushirikiano kati ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali Kuu pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa za Jiji la Dar es Salaam
•Shughuli za kiuchumi kwa jamii katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
•Vyanzo vya Mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na ukusanyaji wake
•Ushirikishwaji wa maoni ya Wananchi katika uongozi
•Juhudi za uhifadhi wa mazingira
•Changamoto zinazoikumba Halmashauri
•Mipango na matarajio ya baadae
•Na masuala mengine ya maendeleo.
Kupitia mawasilisho ya taarifa, Maafisa hao wamepata fursa ya kujifunza kuhusu shughuli za kila siku za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo jijini Dar es Salaam.
Kwa upande mwingine uongozi wa Halmashauri ya Jiji umeeleza mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kipindi cha miaka mitano ikiwemo ujenzi wa miundombinu mbalimbali yenye lengo la kuinua kipato cha wananchi wa Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.