Afisa Ustawi wa Jamii Kanda na. 4 Bi. Suzan Mdesa ameyataka mabaraza ya wazee kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwa na imani nayo kwani Serikali ipo pamoja nao katika kuhakikisha inatekeleza afua mbalimbali kwa ajili ya ustawi wa wazee, hayo yamesemwa leo Oktoba 3, 2024 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Babylon uliopo Kinyerezi.
Aidha, ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inaendelea na juhudi za kuhakikisha Ustawi wa Wazee unaimarika ikiwemo kuimarisha mifumo ili wazee wapate huduma za kijamii kama Afya, ulinzi, usalama na matunzo kwenye makazi ya wazee.
Vilevile, Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo za Afya kwa wazee kwa kutoa kadi maalum zinazowawezesha kupata matibabu bure.
Naye Afisa Ustawi wa Jamii Kata ya Bonyokwa Levina Lucas amewasisitiza wazee hao kuzingatia matumizi ya lishe bora kwa wazee kwa kula mlo kamili huku wakizingatia kuushughulisha mwili kwa kufanya kazi na mazoezi madogomadogo kama kutembea na sio kukaa na kulala.
Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kinyerezi Athumani Mwakibuga ametoa wito kwa wazee hao kujitokeza na kuhamasisha wengine kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajia kufanyika Novemba 27, 2024.
Kaulimbiu ya Siku ya Wazee Duniani 2024 imebeba Kaulimbiu isemayo 'Tuimarishe huduma kwa wazee, wazeeke kwa heshima'
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.