Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewapongeza Watendaji wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Mkurugenzi wa Jiji, Wabunge pamoja na Madiwani kwa namna wanavyofanya kazi kwa bidii na ushirikiano na kubuni vyanzo vya mapato ambavyo huwezesha kupatikana kwa fedha za kufanya miradi ya maendeleo bila kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.
Mhe. Mpogolo ameyasema hayo leo Desemba 20, 2023 alipokuwa kwenye Hafla ya kupokea madawati 17,500 kwa shule za Sekondari zenye upungufu wa madawati ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, hafla iliyofanyika katika shule ya Sekondari ya wavulana Pugu.
"Nawapongeza Watendaji wote wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuendelea kuvunja rekodi katika makusanyo ya mapato na kufikia Bilioni 8 mpaka 10 kwa mwezi tofauti na ilivyokuwa awali na kupitia fedha hizi tunaweza kufanya maendeleo makubwa ikiwemo ununuzi wa madawati haya ambayo tumeyapokea hii leo. Hongereni sana." Amesema Mhe. Mpogolo
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo ameongeza kuwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Kuna upungufu wa madawati 20,000 katika shule za msingi hivyo wamekwishaweka oda ya kutengeneza madawati hayo ili watoto waweze kupata elimu katika mazingira bora Kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Jerry Silaa amempongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya pamoja na Mkurugenzi wa Jiji kwa kazi nzuri wanayoifanya na kuwezesha kupatikana kwa madawati hayo ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kwamba madawati hayo yatatumiwa na watoto wanaosoma elimu bila malipo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.