Na: Hashim Jumbe
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Tarehe 17 Februari, 2025 limefanya Mkutano Maalum wa Mapitio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/25 kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai-Disemba, 2024) na kisha kufanya Makadirio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2025/26 wenye Jumla ya TShs. Bilioni 290.5 ikiwa ni ongezeko la 3.6% ukilinganisha na Bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, kati ya fedha hizo kiasi cha TShs. Bilioni 150.5 sawa na 51.8% ya Bajeti ni Fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu na TShs. Bilioni 140 sawa na 48.2% ya Bajeti ni makusanyo kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Katika Mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Arnatouglou na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto, Baraza la Madiwani lilipokea, likajadili na kisha kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 wenye jumla ya TShs. Bilioni 290.5
Akiwasilisha Rasimu hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya alisema "Kwa mwaka wa fedha 2025/26 Halmashauri imekasimia kukusanya TShs. Bilioni 140 kutoka kwenye mapato yake ya ndani, kati ya fedha hizo Mapato yasiyolindwa ni TShs. Bilioni 101.2 na Mapato lindwa ni TSh. Bilioni 38.7"
Mkurugenzi Elihuruma aliendelea kufafanua "Na kwa upande wa fedha za Ruzuku kutoka Serikali kuu, Halmashauri imeweka makadirio ya TShs. Bilioni 150.5 ambapo Mishahara ni TShs. Bilioni 125.9, Matumizi mengineyo TShs. Bilioni 4.3 na Ruzuku ya Miradi ni TShs. Bilioni 20.1"
Katika Matumizi kwa mwaka wa fedha 2025/26 Halmashauri inakadiria kutumia TShs. Bilioni 140 ya mapato yake ya ndani ambapo mapato yasiyolindwa TShs. Bilioni 101.2 yatatumika kwenye Mishahara TShs. Milioni 721.9 sawa na 0.71%, Matumizi mengineyo TShs. Bilioni 29.6 sawa na 29.28% na Miradi ya Maendeleo TSh. Bilioni 70.8 sawa na 70%, wakati Mapato lindwa ni TSh. Bilioni 38.7.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.