Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 25 Januari, 2020 wakiongozwa na Naibu Meya wa Jiji, Mheshimiwa Abdallah Mtinika kwa kauli moja wamepitisha mpango na bajeti ya mwaka 2020/2021 wa jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 25.3 ikiwa ni bajeti ya mishahara ya watumishi, matumizi ya kawaida na za utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.
Akiwasilisha mpango na bajeti hiyo kwa wakazi na wadau mbalimbali wa Jiji waliohudhuria Mkutano wa Baraza, Naibu Meya Mtinika ameeleza kuwa mpango na bajeti wa shilingi bilioni 25.3 ni kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato na kati ya fedha hizo shilingi za Kitanzania bilioni 13.7 zinatarajiwa kukusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani vya Halmashauri na shilingi za Kitanzania bilioni 11.7 kutoka Serikali Kuu.
Aidha ameeleza kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea kuboresha ukusanyaji mapato yake ya ndani kwa kutumia mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji mapato wa Mamlaka za Serikali za Mitaa pamoja na kubuni vyanzo vingine vya mapato.
Amefafanua kuwa mpango na bajeti ya mwaka 2020/2021 umelenga kutekelaza miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo, barabara na vituo vikuu vya mabasi yaendayo mikoani (Mbezi Luis na Boko), uboreshaji wa miundombinu ya dampo, uwekezaji vitega uchumi kwenye viwanja vya Halmashauri, uendelezaji wa utalii na hifadhi ya mazingira na kuhakikisha utoaji wa huduma bora unaoepusha usumbufu kwa jamii.
Amesema Halmashauri pia imepanga kutumia asilimia 65.72 ya mapato ya ndani sawa na shilingi za kitanzania bilioni 8.1 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya mfuko wa wanawake, vijana na walemavu.
“Makisio ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2020/2021 ya jumla ya shilingi za Kitanzania bilioni 13.7 kutoka katika vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji yameongozeka kwa kiasi cha shilingi za Kitanzania bilioni 5.2 ambayo ni sawa na asilimia 61.77 ya makisio ya shilingi za Kitanzania bilioni 8.4 ya mwaka 2019/2020 kutokana na usimamizi wa karibu, uboreshaji wa mfumo wa ukusanyaji mapato kwa njia ya kielektroniki na kuanza kwa makusanyo kwenye chanzo kipya cha mapato cha Kituo Kikuu cha Mabasi cha mbezi Luis”, alisema Mtinika.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.