Taasisi ya Agrithamani inayojishughulisha na masuala ya Lishe kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Da es Salaam na Wizara ya Kilimo wamezindua programu maalum ya ‘Msosi asilia’ katika hafla maalumu iliyofanyika katika Soko la Kisutu na kuwahusisha mama na baba lishe wa sokoni hapo.
Mradi huo ulioandaliwa na Taasisi hiyo yenye makao yake makuu mjini Bukoba, umefadhiliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na unatarajiwa pia kuzinduliwa katika Miji ya Mbeya na Zanzibar, kwa lengo la kuhamasisha ulaji unaofaa kwa kutumia vyakula vyetu vya kitanzania.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Mobhare Matinyi ametoa shukrani za dhati kwa Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo na Chakula (FAO) kwa ufadhili wa Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya za mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanikisha mradi huu kutekelezwa.
Aidha, amesema kuwa nchi yetu imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inazalisha chakula cha kutosha ili kujihakikishia usalama wa chakula na lishe, hivyo ni laazima nchi yetu iungane na nchi nyingine duniani kuhakikisha inafanya mabadiliko katika mifumo ya chakula ambayo inaanzia kwenye uzalishaji mpaka pale kinapomfikia mlaji.
Pia amesema "Mama na baba lishe ni sekta muhimu hasa kwa wakazi wa mjini, hivyo ni lazima iangaliwe na iboreshwa ili iweze kukidhi mahitaji ya mwili kilishe.”
Taasisi ya Agrithamani kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam chini ya Ufadhili wa Shirika la Chakula na Kilimo duniani imewapa kina mama na baba lishe mafunzo ya umuhimu wa kuandaa vyakula mchanganyiko kupitia makundi mbalimbali ya vyakula ili kuhakikisha walaji wanapata mlo kamili na kuzingatia usafi wa chakula na mazingira ili kulinda afya za walaji.
Ikumbukwe kuwa nchi yetu imepata bahati ya kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa mifumo ya chakula ambao umejumuisha nchi mbalimbali za Afrika hapa Dar es Salaam ili kujadili masuala mbalimbali ya mifumo ya chakula kuanzia tarehe 5 Septemba, 2023 na kuhitimishwa tarehe 9 Septemba, 2023 katika ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.