MSTAHIKI Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amewataka madereva wanaowasafirisha wanafunzi wanaosoma shule nilizopo katikati ya Jiji kuwashusha na kuwachukua ndani ya kuta za shule badala ya kuwashusha na kuwachukua nje.
Meya Mwita aliyasema hayo jijini hapa leo wakati wa uzinduzi wa wiki ya Kimataifa ya usalama barabarani, ambapo pamoja na mambo mengine alisema kuwa utaratibu wanaoutumia madereva hao ni hatari kwa wanafunzi kwani inawalazimu kuvuka barabara.
Alisisitiza kuwa iwapo watatumia utaratibu wa kushusha wanafunzi ndani ya kuta za shule itasaidia kupunguza hatari kwa wanafunzi ikiwemo kugongwa na gari, pikipiki, kupunguza msongamano wa magari barabarani.
“Jambo ambalo linakwenda kufanyika leo ni muhimu sana, limesaidia kuongeza usalama wa watoto wetu ambao wanasoma kwenye shule hizi zilizopo katikati ya Jiji, lakini pia linatoa nafasi kwa walimu kuwa na uhakika wa usalama wa wanafunzi wao, najua wakati mwingine mmekuwa na wasiwasi kuhusu usalama wao.
"Nipende kutoa rai kwa madereva, zingatieni jambo hili, mabasi ya shule yawe yanachukua na kushusha wanafunzi ndani ya kuta za shule, utaratibu ambao mlikuwa mnautumia hivi sasa usitishwe mara moja.
Huko ni kuhatarisha maisha ya wanafunzi ambao baadae wangekuwa madokta, wabunge, marais tunawategemea. Watoto ndio Taifa la kesho, nawaomba sana walimu mlisimamie jambo hilo.
Aidha Meya Mwita aliwataka walimu na shule kwa ujumla kutumia kwa umakini vifaa vya usalama barabarani katika mitaala ya shule ili kuwafundishia wanafunzi masuala ya usalama barabarani kwani kutafanya watambue elimu hiyo na hivyo kuleta manufaa kwa Taifa.
Alisisitiza kuwa "elimu hii ikifundishwa vizuri itapunguza ajali za barabarani wakati wa kuvuka lakini pia hata pikipiki zitaendeshwa kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani bila kuathiri watumiaji wengine wa barabara”.
Hata hivyo Meya Mwita aliwapongeza Automobile Association Of Tanzania (AAT) na Federation International Automobile (FIA) kwa kuchukua jukumu la kupunguza ajali barabarani na kuokoa maisha ya wanafunzi.
Aidha AAT, FIA kwa kushirikiana na kitengo cha Usalama barabarani elimu kwa umma, wamefundisha walimu 1,000 kutoka shule 51 za Jiji la Dar es Salaam kuhusu matumizi sahihi ya alama za barabarani na matumizi sahihi ya barabara ambapo matarajio yake ni kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
Sambamba na hilo, AAT na FIA wameahidi kutoa elimu hiyo kwa kila Halmashuri za Jiji la Dar es Salaam ambapo jumla ya watu 10 watakuwa wakipatiwa mafunzo hayo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.