Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mheshimiwa Edward Mpogolo, amewataka wajumbe wa mabaraza ya kata wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanashirikiana na wananchi katika kusimamia maendeleo na kutatua changamoto kwa njia ya amani.
Akizungumza leo Septemba 26, 2025 wakati wa mafunzo na hafla ya kuwaapisha wajumbe wa mabaraza hayo iliyofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Msingi Kisutu Jijini Dar es salaam
DC Mpogolo amesema wajumbe wanapaswa kuwa mfano wa mshikamano na mshauri sahihi kwa jamii zao.
“Mkafanye suluhu kwa amani. Ninyi ni viongozi wa karibu zaidi na wananchi, hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha mnaweka umoja na mshikamano badala ya migongano isiyo ya lazima, kupitia Elimu mtakayopewa leo isiishie hapa tu hivyo mkaitumie kupunguza migogoro katika jamii na kata zetu." amesisitiza DC Mpogolo.
Sambamba na hilo amewataka wajumbe kuwa wasuluhishi na siyo waamuzi,kwani kwa mujibu wa Sheria ya Mahakama ya Migogoro ya Ardhi sura ya 216, mabaraza ya kata yanasikiliza Migogoro na kusuluhisha na ikishindikana Baraza litatoa hati ya kushindikana usuluhishi wa mgogoro kwa hatua zaidi.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala Bi. Charagwa Sulemani amewataka wajumbe hao, kuwa wavumilivu na kutatua changamoto kwa hekima uadilifu katika kufanya suluhu kwa wananchi katika maeneo yao.
Katika hafla hiyo jumla ya wajumbe 288 kutoka kata 36 za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wameapishwa rasmi na kula kiapo cha uadilifu. Wajumbe hao wameahidi kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Katiba, sheria na kanuni zinazoongoza uendeshaji wa Serikali za Mitaa.
Mabaraza ya Kata ni vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha sheria ya mabaraza ya kata ya mwaka 1985, ambapo kila Baraza linajumuisha wajumbe wasiopungua wanne na wasiozidi wanane watakaochaguliwa na Kamati ya Kata kutoka miongoni mwa majina ya wakazi wa kata yaliorodheshwa kwa kuzingatia taratibu maalum uliowekwa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.