MKURUGENZI wa Halmashauri Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana amesema mradi wa Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika eneo la Mbezi Luis umekamilika kwa asilimia 90 na unatarajia kuanza kutumika rasmi mwishoni mwa mwezi Novemba, 2020.
Liana ameyasema hayo leo tarehe 07 Novemba, 2020 wakati akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la mradi na kuwaeleza hali halisi ya mradi ulipofikia ambapo amesema mradi huo upo katika hatua za mwisho za kukamilika kwake.
“Kama mnavyoona mradi umefikia hatua za mwisho na tarehe 30 ya mwezi huu utakuwa umekamilika kwa hatua ya kwanza kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli aliagiza mradi huo uwe umekamilika hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Novemba” Amesema Liana.
Liana ameongeza kuwa kuanzia tarehe 25 ya mwezi huu mabasi yataanza kutumia Kituo cha Mabasi cha Mbezi Luis huku akiwataka wafanyabishara mbalimbali ambao wanataka kutumia fursa ya kufanya biashara katika Kituo hicho wajitokeza kufanya maombi.
Aidha, Liana amewataka wafanyabiashara ambao wanataka kufanya biashara katika Kituo hicho kuepuka matapeli ambao wanatumia mwanya huo kuwatapeli wafanyabiashara huku akiwasihi waombaji kufuata utaratibu ambao umewekwa wa kuomba kupitia mtandao kupitia anuani www.pangisha.tamisemi.go.tz kuanzia tarehe 09 Novemba, 2020.
Mkurugenzi Liana pia amezungumzia gharama halisi ya mradi huo kuwa ni shilingi za Kitanzania bilioni 50.9 ambazo zilitengwa hapo awali na kufafanua kwamba hakutakuwa na nyongeza ya fedha kwenye mradi huo.
“Nawaambieni mpaka sasa tumeweza kuokoa zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 12 katika hizo bilioni 50.9 zilizotengwa kutokana na usimamizi dhabiti wa mradi huo kwa kuzingatia maelekezo ya Rais Magufuli katika kusimamia fedha za Serikali na sisi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tumesimamia na kuweza kuokoa fedha hizi” Amesema Liana.
Liana ameendelea kueleza kwamba mradi huo ukikamilika utaweza kuingizia mapato Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam zaidi ya shilingi za Kitanzania bilioni 10 kwa mwaka.
Aidha, amesema Kituo Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani katika eneo la Mbezi Luis kitaweza kutoa ajira kwa Watanzania zaidi ya elfu kumi na kuchochea uchumi kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.
Mkurugenzi Liana amehitimisha kwa kueleza changamoto ya ucheleweshaji wa vifaa kulikotokana na mlipuko wa ugonjwa COVID-19 unaotokana na virusi vya CORONA na kupelekea makampuni ya nje kushindwa kuzalisha bidhaa kutokana na ugonjwa huo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.