Na: Doina Mwambagi
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Elihuruma Mabelya amewataka wenyeviti wa Mitaa, watendaji wa Kata, na watendaji wa Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuzingatia sheria na kanuni za kiutumishi.
Ameyasema hayo leo Februari 20, 2025 katika ukumbi wa Lamada uliopo Jijini humu wakati wa kikao kazi maalum kilichowakutanisha wenyeviti wa Mitaa, watendaji wa Kata na watendaji wa Mitaa lengo likiwa ni kupewa maelekezo ya uendeshaji wa shughuli zao.
Mkurugenzi Mabelya amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na mawasiliano mazuri baina ya wenyeviti na watendaji kwa lengo la kuboresha huduma kwa Wananchi.
“Tusitengane, kwa sababu lengo letu ni moja tu, kuwatumikia Wananchi kwa haki na uwazi,na hii itapunguza changamoto zinazojitokeza katika utendaji wetu wa kila siku,” aliongeza Mabelya.
Sambamba na hilo, Mkurugenzi Mabelya amesema Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili viongozi hao ikiwemo kodi za mapango na ubovu wa ofisi na kuwataka Viongozi hao kuwa wavumilivu kwa kuwa Halmashauri imejipanga kufanya ujenzi wa ofisi za kisasa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na kuongeza ufanisi wa utendaji.
Kikao hicho pia kilihudhuriwa na wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Jeshi la Polisi, TAKUKURU pamoja na Mwenyekiti na wajumbe wa Kamati ya Siasa Wilaya ya Ilala.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.