Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo tarehe 20 Novemba, 2023 amefanya mkutano wa hadhara wenye lengo la kusikiliza na kutatua kero za wananchi wa Kata ya Zingiziwa ambapo ameahidi kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali zinazowakabili wananchi hao.
Katika mkutano huo RC Chalamila aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Ilala , wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Viongozi wa Wilaya ya Ilala, Wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na wengine kutoka Taasisi zinazowahudumia wananchi kwa ukaribu ikiwemo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mji (TARURA) , Wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira (DAWASA) pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO).
Akiwa katika kusikiliza kero za wananchi wa Kata ya Zingiziwa, RC Chalamila amepokea changamoto mbalimbali zikiwemo za Elimu, Miundombinu ya barabara, Maji, Umeme, Afya, migogoro mbalimbali ya Ardhi na changamoto za Kisheria ambapo zipo alizotatua papo kwa papo na nyingine kuzipatia utatuzi kwa kuwataka watendaji kuhakikisha wanazishughulikia Mara moja.
Hatahivyo, RC Chalamila amewataka viongozi wa TARURA katika Msimu huu wa mvua kurekebisha miundombinu ya barabara maeneo yenye uhitaji zaidi.
“Niwaombe Wataalamu kutoka TARURA na Halmashauri kuhakikisha msimu huu wa mvua mnrekebisha maeneo ambayo ni muhimu zaidi kwani tusije tukawa tunaweka fedha kwaajili ya kurekebisha miundombinu ya muda mfupi ila ikaharibika zaidi hivyo niwaombe wananchi muwe wavumilivu hadi mvua zitakapoisha ili miundombinu hiyo itengenezwe kwaajili ya matumizi ya muda mrefu”. ameeleza RC Chalamila
Sambamba na hilo RC Chalamila amesema suala la Usalama katika Mkoa wa Dar es Salaam limekua tishio hivyo itafanyika operesheni maalumu kwa baadhi ya maeneo ambayo ni ngome ya vikundi vya uhalifu maarafu kama 'Panya road' lengo likiwa ni kuhakikisha Dar es Salaam inakuwa katika hali ya usalama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Nitoe shukrani zangu kwako Mkuu wa Mkoa kwa kuona haja ya kuja kusikiliza kero za wananchi wa Zingiziwa hivyo nikuhakikishie tutazingatia haki katika kutekeleza yote uliyoagiza pia niwaombe wazazi kuwajibika kwani Serikali inatoa elimu bila malipo hivyo wazazi inabidi muwajibike kuhakikisha watoto wanakula, mkikaa kwenye vikao mkubaliane kupitia kamati zenu kuwa mtatoa kiasi gani kwaajili ya chakula cha watoto. Pia nipende kukuhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa tutahakikisha suala la ulinzi na usalama kwa wananchi wetu linachukuliwa hatua kwa wakati.”
Naye Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Tabu Shaibu amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kutatua kero hizo kwa wakati “Tutahakikisha kero hizi tunazitatua kwa wakati bila kuathiri maeneo mengine kwani Wataalamu wetu tumewaelekeza kufuatilia maeneo yote yenye kero na kushughulikia kwa wakati hususani eneo la elimu, Ustawi wa Jamii, Maendeleo ya Jamii pamoja na eneo la sheria hivyo nipende kutoa shukrani zangu kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa ziara hii ya kutatua kero na nikuhakikishie tumejipanga kuondoa kero za wananchi wa Zingiziwa kwa ajili ya kukuza uchumi wao.”
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa kwa upande wa Soko la Zingiziwa, shedi 5 za kisasa zinatarajiwa kujengwa ambapo ziko hatua ya usanifu na hadi kufikia Disemba 15 Shedi hizo zitakua zimekamilika.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.