Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka mama wajawazito kuzingatia lishe bora kwani lishe bora wakati wa ujauzito ni muhimu sana kwa sababu humpatia mama virutubishi muhimu kulingana na hali yake. Wakati wa ujauzito mama anahitaji virutubishi zaidi kwa ajili ya maendeleo yake kiafya pamoja na mtoto aliyetumboni. Lishe bora huimarisha afya ya mama na humsaidia mtoto kukuwa vizuri kimwili na kiakili.
Mhe. Mpogolo ametoa wito huo leo Juni 6, 2024 wakati wa uzinduzi wa kampeni ya uhamasishaji lishe bora kwa mama wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar ee Salaam Sambamba na kauli mbiu isemayo ‘Lishe bora kwa baba, mama na mtoto ni msingi wa jamii bora na Taifa endelevu’.
Akiongea katika hafla hiyo Mhe. Mpogolo amesema “Taarifa zilizopo zinaonesha hali ya lishe miongoni mwa Watoto hairidhishi kutokana na kuathiriwa na tatizo la udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano, uzito pungufu na ukondefu sasa tunapaswa kuchukua hatua stahiki kusimamia suala zima la watoto lakini pia Lishe bora kwa mama mjamzito hivyo nitoe wito kwa akina baba kushiriki katika kupambania masuala ya lishe kwa watoto wetu kwani Sisi kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha wazazi na walezi wanazingatia lishe bora hii ikiwa ni kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha jamii zetu zinazingatia afua za lishe hivyo zoezi hili linatarajiwa kufanyika kwa wiki moja ya kufanya tafakuri ya lishe ambayo ni lishe ya baba mama na mtoto”.
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha anazoendelea kuzitoa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ya kuboresha miundombinu ya afya ili wananchi wapate huduma bora za Afya kwa wakati huku akieleza kuwa Serikali imeidhinisha shilingi bilioni 21 kwaajili ya ujenzi wa Hospitali tatu katika halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na tayari bilioni 15 zishawekwa na hospitali hizo zitaenda kujengwa eneo la Mnazi Mmoja kwa Jimbo la Ilala, eneo la Pugu kwa Jimbo la Ukonga na Segerea ambapo uwepo wa hospitali hizi utasaidia huduma za afya kupatikana kwa wakati.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam Dkt. Zaituni Hamza ameeleza kuwa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii imeendelea kutekeleza maagizo ya kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa, lishe inazingatiwa pamoja na kupunguza vifo vya mama wajawazito kwani katika kutekeleza hayo Idara imekua ikifanya semina mbalimbali kuhusu lishe kwa mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano, huduma za mawasiliano zimeboreshwa kwani Idara imeweka namba ya dharura endapo mjamzito atapata changamoto atazitumia ili kupata huduma kwa uharaka hii itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto pia katika hafla hiyo idara inaenda kuwapatia Kadi za CHIF watoto chini ya miaka mitano wanaoishi katika mazingira magumu hii inaonyesha ni jinsi gani idara inatekeleza maagizo ya kuboresha huduma za afya pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya kwa wakati.
Aidha, katika Hafla hiyo kulikua na uzinduzi wa chanjo ya matone ya vitamini A pamoja na ugawaji wa mavazi ya uzazi (maternity Dress) kwa wamama wajawazito wasiopungua 100 na wanaonyonyesha zenye ujumbe usemao ‘asante mama Samia mimi na mtoto tuko salama’.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.