Katika kuelekea Siku ya Upandaji Miti ambayo hufanyika Kitaifa kila tarehe 01, Aprili, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Jonas Mpogolo leo Machi 29, 2023 amefanya kikao na waandishi wa habari lengo likiwa ni kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha Umma juu ya upandaji wa miti hasa katika kipindi hichi cha mvua.
Akizungumza katika Kikao hicho Mhe. Mpogolo amesema ”Lengo la mkutano huu ni kuhabarisha, kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa Wilaya ya Ilala kupanda miti kwa wingi hasa kipindi hichi cha mvua kwani kauli mbiu ya mwaka huu katika siku ya mazingira ni ‘Misitu ni Afya’ hivyo kutokana na kauli mbiu hii Inabidi tupande miti kwa wingi kwa afya na kwa kukuza uchumi pia, Sisi kama Wilaya tumedhamiria kupanda miti Takribani milioni 1.5 kama alivyoelekeza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philp Isdori Mpango mnamo Novemba 2022 akiwa Mbeya kuwa kila Halmashauri wahakikishe wanapanda miti takribani milioni 1.5 hivyo sisi tunatekeleza hilo ambapo kwa mwaka 2022 tuliweza kupanda takribani miti milioni 1.3 hivyo na mwaka 2023 tutahakikisha tunapanda miti milioni 1.5 katika baadhi ya maeneo yetu mabalimbali”.
Aidha Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa kutokana na Kauli mbiu ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishirikiana pamoja na Mkuu wa Mkoa ya ‘Mti wangu’ Wilaya ya Ilala watahamasisha zoezi la upandaji miti katika Shule za Msingi na Sekondari ambazo zina takribani wanafunzi laki 4 ambapo kila mwanafunzi akipanda mti wake zoezi hilo litakua limekamilika kwa kiasi kikubwa.
vilevile Mhe. Mpogolo amewataka viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata kuhakikisha wanawahimiza wananchi wao kupanda miti kwa wingi huku akiwataka watu wenye majengo pembezoni mwa barabara pamoja na viwanda kuhakikisha wanapanda miti kwenye vungu na kuviweka mbele ya majengo yao ili kupendezesha mazingira na kuvutia mandhari ya Jiji letu la Dar es Salaam ambalo ndio kitovu cha wageni wengi wanapoingia Nchini Tanzania.
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo ameeleza kuwa kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam itapanda miti ya matunda pamoja na miti ya kivuli hususani maeneo ya Mashuleni, pembezoni mwa barabara zetu na miti mingine itapandwa pembezoni mwa bonde la mto Msimbazi "Kwa upande wetu Jiji la Dar es Salaam tutashirikiana na Wenzetu wa TFS kwani wameahidi kushirikiana na sisi katika kupendezeshanmazingira yetu hivyo wameahidi kutupatia miche ya miti mbalimbali inayoweza kupandwa katika Jiji letu.”
Aidha Mhe. Mpogolo ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi kwani sheria ya saivi inamtaka mwananchi atenge asilimia 5 ya ardhi yake kuwa kijani hivyo ametaka Idara ya Mazingira ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wana kitalu cha miti kwani wataalamu wapo ambao watasaidiana nao kukamilisha jambo hilo la kupendezesha mazingira .
Kwa upande mwingine Mhe. Mpogolo alihitimisha kwa kuwataka wananchi kuchukua tahadhari kipindi hichi cha mvua hasa wanapovuka katika maeneo ya mito huku akitoa maagizo kwa Viongozi wa Serikali za Mitaa na Kata kuhakikisha wanachukua hatua za kisheria kwa wananchi wote wanaotiririsha maji taka wakati wa mvua hivyo kwa wananchi wote waliounganisha mfumo wa maji taka na mfumo wa maji ya mvua wahakikishe wanaacha tabia hiyo kwani wanachafua mazingira.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.