Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mussa Azzan Zungu amewataka wajasiriamali kuwekeza kwenye miradi ya kilimo kama sehemu ya ujasiriamali wao, hayo ameyabainisha leo wakati akifunga Maonesho ya siku tatu ya Wajasiriamali yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala chini ya Programu ya Imbeju.
Akiongea wakati wa Kufunga maonesho hayo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam Mhe. Zungu amesema “Niwashukuru sana CRDB Bank kwa mchango huu mkubwa wa kuendelea kuinua wajasiriamali ikiwa ni sehemu ya kuwapa vijana na wanawake ajira. Hivyo niwaombe Mikopo mnayoitoa iwe na riba ndogo ili kuzidi kuhamasisha wajasiriamali katika shughuli zao za kukuza uchumi wao na wananchi kwa ujumla. Pia nipende kutoa wito kwa wajasiriamali wote msiache kujihusisha na miradi ya kilimo kwa mikopo inayotolewa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na benki mbalimbali hivyo ni vyema mkajihusisha pia miradi hiyo ili kupata fursa zaidi ya hizi lzitakazo wakwamua Kiuchumi.”
Smbamba na hilo Mhe. Zungu ametoa agizo kuwa wagambo wote wakorofi wanaowaonea wafanyabiashara wakamatwe ili wananchi wawe na amani kwani amani ni dhana muhimu kwa kila Mtanzania wakawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema “Jambo hili lilikua wazo na sasa limekua kweli hivyo niwashukuru sanaCRDB Bank kwa kukubali kushirikiana nasi kuwezesha maonesho haya hivyo kwaniaba ya Serikali niwashukuru wajasiriamali kwa kuitikia na kuonesha muamko mkubwa na ninaamini wakati mwingine tutaboresha maonesho haya ya endelevu kuwa bora zaidi ya hapa.”
Naye Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bi. Fransisca Makoye ameeleza kuwa “Tukiwa na dhamana ya kusimamia wajasiriamali kama Idara tumeweza kufanya tathmini ya maonesho haya kuanzia tarehe 11 hadi leo hii tarehe 13 ambapo wajasiriamali waliweza kutoa maoni yao kuwa siku za maonesho haya ziongezwe kutoka siku tatu hadi saba huku zaidi ya asilimia 9% ya wahasiriamali waliweza kuelewa elimu waliyopewa juu ya mambo mbalimbali hivyo nizishukuru Taasisi zote zilizoungana nasi kwa siku tatu hizi kutoa elimu kwa wajasiriamali kwani wajasiriamali hawa wamepata fursa ya kutambulisha biashara zao na kupata fursa zaidi.”
Maonesho hayo ya siku tatu (tarehe 11-13 Septemba, 2023) yaliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya yamefanyika kwenye Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam yakiwa na lengo la kutoa muamko kwa wajasiriamali ili waweze kuchangamkia fursa mbalimbali zinazopatikana baada ya kujiunga na majukwaa mbalimbali yanayoambatana na elimu ya ujasiriamali.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.