Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri za Manispaa za Jiji la Dar es Salaam leo tarehe 16 Desemba, 2020 katika ukumbi wa Karimjee wamemchagua Diwani wa Kata ya Tabata Mheshimiwa Omary Abdallah Matulanga kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam ndugu Paulo Mshimo Makanza, amesema uchaguzi wa Meya wa Jiji umehudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani 140 kati ya 154 na kura zilizopigwa ni 140 ambapo kura za ndio zilikuwa 140 na hakukuwa na kura za hapana.
“Hivyo basi kwa mujibu wa Kanuni 13 (7) ya Kanuni za Kudumu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Tangazo la Serikali namba 417 la mwaka 2015 napenda kumtangaza ndugu Omary Abdallah Matulanga kuwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam”, Amesema Makanza.
Aidha, Makanza amefafanua kwamba Meya huyo mteule anatarajia kuapishwa Desemba 23 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine utafanyika Mkutano wa kwanza wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, kuapishwa kwa Waheshimiwa Madiwani pamoja na Uchaguzi wa Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mstahiki Meya mteule Mheshimiwa Matulanga ametoa shukrani kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kumchagua kwenye nafasi hiyo huku pia akitoa pongezi kwa Waheshimiwa Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam waliompigia kura za ndio na kumpa fursa ya kuongoza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
“Nina imani lengo letu kwa pamoja ni kuhakikisha Jiji hili linapiga hatua katika maendeleo na kuhakikisha tunafanikisha malengo ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ya kuwaletea Watanzania maendeleo”, Amesema Matulanga.
Naye Katibu wa CCM mkoa wa Dar es Salaam, ndugu Adam Ngalawa, amewataka Waheshimiwa Madiwani kuhakikisha wanasimamia kwa nguvu zote katika kutekeleza ilani ya chama hicho na kusisitiza kusiwe na migongano katika kusimamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.