Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila ameipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa uboreshaji wa mazingira katikati ya Mji lengo likiwa ni kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakua safi sambamaba na madhari nzuri.
Mhe. Chalamila ametoa Pongezi hizo leo Mei 29, 2024 wakati akiendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Jiji la Dar es Salaam katika Jimbo la Ilala, ambapo aliweza kukagua maeneo manne ya Kata ya Kivukoni ikiwemo Ujenzi wa barabara ya Mindu,Mradi wa Perving mtaa wa Ohio na Karimjee pamoja na kukagua mradi wa uzibuaji mitaro eneo ya IT-Plaza.
Akiongea na wananchi na wafanyabiashara waliokuwepo maeneo hayo, Mhe. Chalamila ameeleza kuwa kutokana na mazingira ya Mjini kati kuwa katika hali isiyo ridhisha, Jiji la Dar es Salaam limechukua hatua stahiki ya kuhakikisha mazingira ya Mji yanakua safi na mandhari ya Jiji inapendeza kwani Dar es Salaam ndio kitovu cha kupokea wageni na mikutano mingi ya Kimataifa inafanyikia katikati ya Miji hivyo uboreshaji wa mazingira hayo ni chachu ya kuvutia wageni katika Jiji la DSM.
“Nipende kuipongeza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa Hatua waliyoichukua ya kuboresha Jiji letu kwa kuweka perving na Kupanda miti na maua katika maeneo ya katikati ya Mji jambo linalofanya mandhari ya Jiji kuwa safi na kupendeza hivyo niwasisitize wafanyabiashara wote pamoja taasisi zote kutambua kuwa wajibu wao ni kuhakikisha Mji unakua safi pia napenda kuwapongeza Viongozi wa Jiji kwa kuchukua hatua ya kuzibua mitaro katika maeneo yaliyokua yanajaa maji wakati wa mvua kwani jitihada hizo zimepelekea kugundua kuwa kuna watu wanatiririsha maji machafu katika mifumo ya maji taka jambo ambalo linasababisha uchafu wa mazingira na kupelekea uwepo wa magonjwa ya milipuko, Sambamba na hilo nitaandaa kikao kazi kuzungumza na Watendaji wa Kata juu ya upendezeshaji wa Mji pamoja na kuongea na wadau na wamiliki wa majengo yote yalioko pembezoni mwa bararabara kutoka Airport hadi kufika Ikulu tuone namna gani tutapendezesha Jiji letu kwa kupanda miti pembezoni mwa barabara”.
Sambamba na hilo, Mhe. Chalamila amewataka PSSF pamoja na Ubalozi wa Canada kuhakisha ndani ya wiki moja wahakikishe wanatenganisha mfumo wa maji taka kwenye mfumo wa maji safi huku akiwataka wafanyabiashara wanaofanya biashara pembezoni mwa barabara katikati ya Mji waondoke na watafutiwe mahali sahihi pakufanya biashara zao ambapo wafanyabiashara wanaotambulika na sio kufanya biashara katika maeneo ya pembezoni mwa barabara ambayo ni mahususi kwaajili ya watembea kwa miguu.
Vilevile, Mhe. Chalamila ameweza kukagua ujenzi wa barabara ya Lindi ambapo amewaagiza Mamlaka ya Maji safi na Maji taka Dar es Salaam( DAWASA) wahakikishe wanashughulikia tatizo la maji taka katika barabara ya Lindi ambayo yamekuwa kero kwa Wananchi wa Kata ya Ilala na wafanyabiashara wanaozunguka eneo hilo huku akiwataka Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) kuhakikisha ndani ya wiki moja Mkandarasi anayetekelezaujenzi wa barabara ya Lindi anaanza ujenzi.
Awali akizungumza wakati wa Ziara hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amesema “Baada ya kuona changamoto yaJiji la Dar es Salaam baadhi ya maeneo yanajaa maji wakati wa mvua tulichukua hatua stahiki za kuzibua mitaro maeneo ya Kamata, CBE pamoja na Muhimbili ambapo tulibaini baadhi ya majengo makubwa mifumo yao ya maji taka imeunganishwa kwenye mifumo ya maji safi, pia maeneo yote ya katikati ya mji yaliyowekwa pavings tunayatangaza kama Smart area na haturuhusu biashara yoyote kufanyika, hivyo nipende kukushukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara hii ndani ya Jimbo la Ilala kwani sisi kama Wilaya ya Ilala tutahakikisha mazingira ndani ya Jiji letu yanakua safi na tutaendelea kutekeleza yale yote uliyotuagiza lengo likiwa ni kuunga Mkono Juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupendezesha Miji na kuwapanga wafanya biashara katika maeneo yao”.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo Cha Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Bi. Theresia Dennis ameeleza kuwa Jiji la Dar es Salaam liko katika kampeni ya uboreshaji wa mandhari katika maeneo yake ambapo shilingi bilioni 1.1 zimetumika kuboresha mandhari ya Jiji katika maeneo 9 ya katikati ya Mji kuwekewa pavings pamoja na upandaji wa miti huku utekelezaji wa mradi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 95.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.