Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Albert Chalamila leo Mei 28, 2024 amefanya ziara katika Jimbo la Ukonga ambapo amekagua miradi mitatu ikiwemo barabara ya Kitunda-Kivule-Msongola ,Hospitali ya Wilaya Kivule pamoja na ukaguzi wa tanki la maji lililopo Bangulo.
Akijibu maswali ya Wananchi wakati wa ukaguzi wa Barabara ya Kitunda-Kivule-Msingola, Mhe. Chalamila amesema Serikali inatambua changamoto ya Barabara hiyo ambayo imekuwa kero kwa Wananchi na kusema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe .Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia barabara hiyo iweze kujengewa kwa kiwango cha zege na utekelezaji kuanza Julai 2024.
Sambamba na hilo Mhe. Chalamila amewataka Wananchi wa Kata ya Kivule pamoja na Kitunda kuacha tabia ya kujenga mabondeni hali inayosababisha kujaa kwa maji katika makazi hayo na kuziba mitaro ya maji katika barabara.
"Kuna baadhi ya Wananchi wamekuwa na tabia ya kujenga kwenye maeneo ya barabara ambayo hupelekea njia za maji kuziba na hivyo mvua ikinyesha maji huingia barabarani, nipende kutoa rai yangi kwa Wananchi kuwa mara baada ya ukarabati, ujenzi utakapoanza kila mtanzania ajilinde mwenyewe kama amejenga eneo la barabara apishe ujenzi na ikitokea mwananchi kukiuka hilo hatua stahiki zitachukuliwa”. Amesisitiza Mhe. Chalamila
Aidha Mhe. Chalamila pia aliweza kukagua ujenzi wa jengo la Wazazi katika Hospitali ya Wilaya Kivule ambapo aliwataka Wananchi kutumia miundombinu iliyopo huku akiwahakikishia kukamilika kwa miundombinu ya barabara kwani Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu ameboresha na anendelea kuboresha miundombinu ya afya ili kuendelea kuwasogezea wananchi huduma za afya kwa ukaribu zaidi.
Vilevile Mhe. Chalamila aliweza kukagua tanki la maji lililopo Bangulo ambapo aliwaeleza wananchi adhma ya Serikali ni kuziondoa Changamoto zinazowakabili ikiwemo maji, umeme, urasimishaji na barabara ambapo amewahakikishia Serikali ni sikivu, kero zao zote zitaisha.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa ziara yake ya kukagua miradi pamoja na kuongea na wananchi katika maeneo yote aliyokagua huku akimuhakikishia kutekeleza yale yote aliyoyaagiza.
Naye Meneja wa Tarura Mkoa wa Dar es Salaam Eng. John Magoli ameeleza kuwa barabara ya Kitunda-Kivule kuelekea Msongola ina Kilometa 16 ambapo Mei 31, 2024 zabuni itafunguliwa na Julai 2024 ujenzi wa barabarara hiyo utaanza kutekelezwa kwa kiwango cha zege.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.