Na: Shalua Mpanda
Katika kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linakuwa salama na kuwezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa saa 24, Halmashauri ya Jiji hili limetenga kiasi cha Shilingi Milioni 514 kwa ajili ya kufunga kamera za usalama (CCTV cameras) katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza wakati wa halfla ya utiaji saini mikataba zaidi ya mitatu ya miradi mbalimbali iliyofanyika katika viwanja vya Karimjee leo Februari 18,2025, Mkurugenzi wa Jiji hili Elihuruma Mabelya amesema hatua hii ina lengo la kudhibiti vitendo vya uhalifu na kusaidia vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Mkurugenzi huyo amesema ufungaji wa kamera hizo utaongeza wigo wa wafanyabiashara kukuza mitaji yao kutokana na kuweza kufanya biashara zao nyakati zote bila kuhofia usalama wao na mali zao.
"Lengo la Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ni wafanyabiashara wafanye biashara zao usiku na mchana,lakini haya yote hayawezi kufanyika kama wafanyabiashara hawatakuwa na uhakika wa ulinzi na usalama". Alisema Mabelya.
Awali akielezea mradi huo, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ndugu Kitutu Mshana amesema pamoja na ufungaji wa kamera hizo ambapo kwa awamu ya kwanza zitafungwa kamera 40, pia kutakuwa na usimikwaji wa mifumo mbalimbali itakayoendesha kamera hizo.
Sambamba na Mkataba huo ambao Halmashauri ya Jiji umeingia na Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), pia imetiliana saini mkataba na Kampuni ya Kajenjere wa uzoaji wa taka pamoja na mkataba wa ujenzi wa shule ya Sekondari Bonyokwa na kampuni ya Platnum .
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.