Na: Shalua Mpanda
Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Elihuruma Mabelya amesema Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji wamedhamiria kuzifanyia ukarabati barabara na makaravati yaliyoathiriwa na mvua zinazoendelea kunyeesha katika maeneo mbalimbali.
Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kukagua maeneo yalioathiriwa na mvua hizo katika kata za Mzinga na Kivule huku akisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu imekuwa ikitoa fedha nyingi kila mwaka katika miundombinu ya barabara ndani ya Halmashauri hii.
"Leo hii tumefanya ziara katika eneo hili la daraja la Mzinga ambalo kwa siku kadhaa lilikuwa halipitiki kutokana na kukatika baada ya maji kukata eneo la barabara hii,niwahakikishie Halmashauri ya Jiji inachukua hatua za haraka kuhakikisha inarekebisha barabara zote zilizopata changamoto kama hii iii wananchi waendelee na shughuli zao za kuzalisha uchumi'. Alisisitiza.
Akiwa katika eneo la barabara ya Pugu Majohe Mbondole, Mkurugenzi huyo amesema Halmashauri ya Jiji kupitia fedha za mapato yake ya ndani imeshaanza ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa mita 400 na mchakato unaendelea kuhakikisha barabara hiyo yenye urefu wa takribani kilometa 12 inajengwa kwa kiwango cha lami kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).
Kwa upande wake Meneja wa TARURA wilaya ya Ilala Mhandisi John Magori amesema kiasi cha kilomita 400 za barabara za kiwango cha lami zimejengwa na Halmashauri kupitia fedha za mapato yake ya ndani.
Aidha Mhandisi huyo amewaomba wananchi kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mvua ambapo barabara nyingi zinakuwa na changamoto kutokana na maeneo maji kuharibu miundombinu hiyo huku akisisitiza kufanya kazi usiku na mchana kukabiliana na changamoto hiyo.
Ziara hiyo pia ilimhusisha Mkuu wa wilaya ya Ilala Mheshimiwa Edward Mpogolo ambaye amekuwa mstari wa mbele kila mara kufika kwa wakati kila inapotokea dharura hasa katika miundombinu ya barabara.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.