Na Doina Mwambagi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, ameuhakikishia uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ilala kuwa yeye pamoja na wataalamu wa Jiji hilo wataendelea kusimamia miradi ya maendeleo hadi ikamilike kwa ubora na kwa wakati.
Mkurugenzi Mabelya ametoa kauli hiyo leo Juni 19, 2025 wakati wa Mkutano Maalum wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ilala, uliolenga kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho kwa kipindi cha miezi sita, uliofanyika katika ukumbi wa Karimjee jijini humo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mabelya amesisitiza kuwa licha ya asilimia kubwa ya Ilani ya CCM kutekelezwa, bado wanayo dhamira ya kuhakikisha miradi yote iliyosalia inakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.
“Pamoja na kukamilika kwa asilimia kubwa kwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, sisi kama Watendaji hatutaacha kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo. Tumeshachukua hatua madhubuti kuhakikisha miradi iliyokwama inakamilika kwa ubora na kwa wakati uliopangwa. Tayari mikataba 19 ya miradi iliyokuwa inasuasua imevunjwa bila kuisababishia Serikali hasara yoyote,” amesisitiza Mkurugenzi Mabelya.
Aidha, amesema licha ya kuwepo kwa changamoto za barabara, Halmashauri kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya na Mstahiki Meya, imechukua hatua madhubuti kwa kutekeleza agizo la Serikali la kuelekeza asilimia 10 ya mapato ya ndani kwenye miradi ya barabara, ambapo fedha hizo zitatumika kwa ukarabati na ujenzi wa barabara katika kata zote 36 na mitaa 159 ya Jiji.
Halmashauri ya Jiji inaendelea kujizatiti kuhakikisha miradi yote inaleta matokeo chanya maslahi mapana ya wananchi wake.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.