Ujumbe wa wanafunzi 15 kutoka Chuo Kikuu cha New York nchini Marekani wakiongozwa na walimu wao, Profesa Jens Rudbeck na Profesa Barbara Borst, wametembelea Jengo la kihistoria la Old Boma katika Jiji la Dar es Salaam tarehe 07 Juni, 2018 na kushangazwa na mambo mengi ya kuvutia waliyoyakuta katika jengo hilo nje ya matarajio yao.
Kati ya mambo yaliyowashangaza wanafunzi hao ni juhudi zilizofanywa na Serikali kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuvionesha vivutio vyake vya utalii na uhifadhi wa majengo ya kihistoria katika Jiji hilo kwa kushirikiana na wadau kama vile Dar es Salaam Centre for Architectural Heritage(DARCH) na Jumuiya ya Wabunifu Majengo Tanzania (Architect Association of Tanzania) ambapo matokeo yake halisi yameonekana kupitia jengo la Old Boma kwa ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya.
Katika jengo hilo ambalo ni Makumbusho ya Jiji la Dar es Salaam wanafunzi hao waliweza kupata historia yote ya Jiji la Dar es Salaam ikiwemo ya uhifadhi ya majengo na mambo ya kale na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii katika jengo hilo ambalo linaendelea kuwa kivutio kikubwa cha utalii ndani na nje ya nchi. Hivi karibuni wanafunzi wapatao 35 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam walifanya ziara ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii katika Jiji hilo likiwemo Jengo hilo la Old Boma.
Ziara ya wananfunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilikuwa ni ya kwanza kufanyika kwa madhumuni ya kukuza utalii wa ndani mara baada ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Suleiman Jafo(Mb) kuzindua rasmi shughuli za kukuza utalii katika Jiji hilo kupitia Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit), huduma za usafari zinazotolewa kupitia mradi huo na ukuwaji wa kasi wa Jiji la Dar es Salaam navyo vimekuwa ni sehemu ya vivutio vikubwa vya utalii kwa wanafunzi hao wa Chuo Kikuu cha New York.
Viongozi wa ujumbe huo, Profesa Rudbeck na Profesa Borst, kwa pamoja wameishukuru Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa kufanikisha ziara yao na kuonesha nia ya kutembelea tena Dar es Salaam na wanafunzi wengine. Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Waziri Kombo, ametoa wito kwa ujumbe huo kuwa mabalozi wa Jiji la Dar es Salaam wa kuvitangaza vivutio vya utalii vya Jiji hilo katika sehemu mbalimbali nchini Marekani.
Ujumbe huo uliowasili nchini tarehe 04 Juni, mwaka huu unatarajiwa kurejea nchini Marekani tarehe 08 Juni, mwaka huu ukiwa umefurahishwa na maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam, hususan juhudi zinazofanywa na Serikali kukabiliana na changamoto zinajitokeza katika eneo la mipango miji, ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, huduma za elimu na mpango wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wa kukuza utalii.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.