Na: Rosetha Gange na Judith Damas
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla leo Tarehe 21 Juni 2021 amewaapisha Wakuu wapya wa Wilaya walioteuliwa tarehe 19 Juni 2021 na Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan katika ukumbi wa Arnatoglou uliopo Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ya uapisho iliwajumuisha Wakuu wote wa Wilaya tano(5) za Mkoa wa Dar es Salaam,ambapo Wakuu wa Wilaya wawili ambao ni wapya waliweza kuapa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Mhe. Fatma Almas Nyangasa na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe.Kheri Denice James. Wakuu wa Wilaya Waliosalia hawakuweza kuapa kwa kuwa wawili walibadilishwa vituo vya kazi akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe ambae sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Jokate Urban Mwegelo na aliyekuwa MKuu wa Wilaya ya Temeke ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe.Godwin Crydon Gondwe huku Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe.Ng’wilabuzu Ndwata Ludigija akibaki katika Wilaya aliyopangiwa awali.
Akizungumza na Wakuu wa Wilaya Wateule baada ya uapisho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe.Amos Makala alitoa pongezi kwa Wakuu wa Wilaya wapya na kumshukuru Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi alioufanya.
Aidha, Mhe. Makalla aliweza kuwaelekeza Wakuu wa Wilaya hao vipaumbele vyake katika utendaji wa kazi ikiwemo ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kuwahudumia Wananchi wake na kuleta maendeleo katika Taifa, usikilizaji na utatuzi wa kero za Wananchi kuanzia Ngazi ya Mtaa mpaka katika Halmashauri zao,kusimamia ulinzi na usalama kwa kuweka mikakati ya kudhibiti Uhalifu, kusimamia usafi wa mazingira ili kuweka Mkoa katika hali ya usfi pamoja na usimamizi,ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.Sambamba na hayo amesema; “Nendeni mkatimize wajibu wenu ipasavyo na mkatekeleze matarajio ya Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kwani amewaamini na ndio maana amewapa nafasi hizo.”
Akitoa neno la Shukurani kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya wengine, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watendaji wenzake pamoja na kuyapokea maagizo yote yaliyoagizwa na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam vilevile kuyatekeleza majukumu yao yote kwa weledi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.