Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wamefanya ziara ya mafunzo ya siku nne kuanzia Juni 4 hadi Juni 8, 2024 Nchini Rwanda lengo likiwa ni kubadilishana uzoefu katika masuala ya Elimu.
Aidha, mafunzo hayo yanayolenga kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi katika Jiji la Dar es Salaam, yamehudhuriwa na Walimu Wakuu 48 kutoka Shule zote za Msingi za Jiji la Dar es Salaam na yanasimamiwa na Taasisi ya Rwanda Cooperation chini ya Wizara ya Mambo ya Nje Nchini Rwanda.
Kwa upande wake Mratibu wa Mafunzo hayo Mwl. Simon Mndendemi ameeleza kuwa “Mafunzo haya yamekua ni chachu ya mafanikio kwetu kwani tumejifunza mambo mengi ikiwemo matumizi ya ICT katika kufundishia na kujifunza, jinsi ya kupunguza mdondoko wa wanafunzi, mbinu za kisasa na kufundishia, utunzaji na uhifadhi wa mazingira, programu ya lishe shuleni, ushiriki wa jamii katika kuchangia Elimu, utamaduni unavyoweza kutumika katika kukuza umoja ,uzalendo na uwajibikaji pamoja na ubunifu na uendelezaji wa vipaji vya watoto, uboreshaji wa madarasa (smart classrooms) hivyo kutokana na mada hizi nimatumaini yangu tunaenda kuboresha elimu yetu”.
Sambamba na hilo, Mwl. Mndendemi amemshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa kuwawezesha kushiriki mafunzo haya huku akiaahidi kuwa kupitia mafunzo hayo watahakikisha wapunguza tatizo la utoro kwa wanafunzi, watawajali Walimu wengine kwa kutoa motisha kwa Walimu na wanafunzi ili kuongeza ufaulu, wataweka mkazo katika kufundisha kwa njia ya vitendo zaidi kuliko nadharia , wataanzisha Programu za kutambua vipaji vya watoto, kuwatia moyo na kuviendeleza vipaji vyao bila kusahau kuweka mkazo katika matumizi ya vifaa vya TEHAMA kwa walimu na wanafunzi pamoja na kushirikisha jamii katika programu ya utoaji wa chakula shuleni na maendeleo ya shule yote haya yatasaidia kuboresha elimu na kuongeza ufaulu kwa shule za Msingi za Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, akiongea kwa niaba ya Walimu wenzake Mwl. Anthony Everiste kutoka Rwanda amefurahishwa na ujio huo ambao umekua chachu ya wao kubadilishana uzoefu na kujifunza kwani kupitia mafunzo hayo wameweza kujifunza jinsi tunavyotekeleza mpango mkakati wa ujifunzaji (KPI) huku wakiipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna wanavyowajali Walimu kwani kwenye nchi yao haijawahi kutokea walimu wakapewa fursa ya kujifunza nchi nyingine.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.