Wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Olympio iliyopo Manispaa ya Ilala katika Jiji la Dar es Salaam, Johari Saleh na Anitha Masangula, wamepata fursa ya kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa siku saba na wanafunzi wenzao katika mji wa Strangnas nchini Sweden.
Johari, mwanafunzi wa darasa la sita na Anitha, mwanafunzi wa darasa la tano, wapo nchini Sweden kuanzia tarehe 25 Mei, mwaka huu kujifunza namna ya kutimiza wajibu wao kama wanafunzi kupitia mabaraza ya wanafunzi na mabaraza ya vijana kwa maslahi ya wanafunzi na vijana ikiwa ni sehemu ya wajibu wao katika ujenzi wa taifa.
Strangnas na Jiji la Dar es Salaam, kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Sweden(SIDA), wamekubaliana kuanzisha, kuboresha na kuimarisha mabaraza ya wanafunzi kama chombo kitakachowasaidia wanafunzi, chini ya ulezi wa walimu wao na Halmahauri zao za Manispaa, kutoa maoni yao kuhusu uboreshaji wa huduma na miundominu muhimu itakayochochea mafanikio yao katika elimu, kuwa viongozi bora na raia wenye uzalendo kwa nchi yao.
Nchini Sweden wanafunzi hao wanatembelea baadhi ya shule za msingi zenye mabaraza hayo na kubadilishana uzoefu na walimu na wanafunzi wenzao, kwa kuzingatia misingi ya demokrasia inayowapa uhuru wa kuwasilisha mawazo yao kama wanafunzi katika uongozi wa shule zao.
Johari na Anitha wameweza pia kukutana na baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Strangnas na kushiriki katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani wa Jiji hilo.
Shule za Msingi zilizomo katika mpango huo katika Manispaa ya Ilala ni Olympio, Zanaki na Kisutu.
Kwa uratibu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Strangnas, Manispaa ya Ilala bado ina fursa kubwa ya kuwawezesha wanafunzi wengine kujifunza nchini Sweden na wale wa Sweden kufanya ziara ya kujifunza nchini Tanzania.
Ufadhili wa SIDA kupitia mradi wake wa "Youth Democracy" una lengo la kuimarisha mabaraza ya wanafunzi na vijana ili kuwaandaa kuanzia ngazi ya Shule ya Msingi kuelewa na kutekeleza wajibu wao katika taifa lao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.