Katika kuendeleza dhamira yake ya kuhakikisha Elimu ya Lishe inatolewa katika maeneo yote na watu wa rika na makundi yote, Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeendelea na utoaji wa elimu ambapo leo tarehe 19 Desemba, 2024 imetoa elimu kwa wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini.
Akiongea wakati wa utoaji wa elimu hiyo iliyotolewa kwenye Shule ya Sekondari Majani ya Chai, Kaimu Mratibu wa Lishe wa Jiji la DSM Neema Mwakasege amesema lengo la elimu hii ni kuhakikisha wananchi wanakuwa na uelewa wa mlo kamili uliozingatia makundi sita ya vyakula.
"Lishe bora ni kula chakula cha kutosha na chakula chenye virutubisho vyote muhimu. Lishe bora husaidia mwili kukua vyema, kuujenga mwili lakini pia huimarisha kinga ya mwili ili kuweza kupigana na magonjwa. Ili lishe iwe bora ni muhimu iwe na mchanganyiko wa Makundi sita ya chakula ambayo ni protini, wanga, fati, mbogamboga, madini, matunda na maji kwa wingi hivyo tuhakikishe tunawapa watoto mlo kamili lengo likiwa ni kupunguza udumavu na kuongeza uelewa kwa watoto kwani lishe bora ndio msingi wa makuzi bora ya kimwili." Amesema Bi. Mwakasege.
Kwa upande wake Afisa Lishe Neema Manyama alisisitiza ulaji wa mlo kamili wakati wa ujauzito na unyonyeshaji kwani Ukosefu wa lishe bora huweza kusababisha matatizo mbalimbali ya kiafya kama vile mama kutoongezeka uzito kama inavyotakiwa na hivyo kukosa nguvu, upungufu wa damu wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ambao huweza kusababisha kifo, uwezekano wa mimba kuharibika, mtoto kufia tumboni, kuzaa mtoto mwenye uzito pungufu, kuzaa mtoto njiti au kuzaa mtoto mfu na kuongezeka kwa magonjwa kwa sababu ya mfumo wa kinga kuwa dhaifu.
Naye Bi. Happy Kanda alitoa elimu kuhusu Makuzi, malezi na maendeleo ya awali ya mtoto.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.