Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Elihuruma Mabelya amewataka wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kufuata maelekezo na sio kufanya kazi kwa mazoea huku akisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu na kanuni ili kuepusha sintofahamu zinazoweza kujitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajia kufanyika November 27,2024 Sambamba na kauli mbiu isemayo "Serikali za Mitaa sauti ya Wananchi jitokeze kushiriki Uchaguzi".
Wito huo umetolewa leo Oktoba Mosi, 2024 wakati wa ufunguzi wa semina ya mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi kwa ngazi ya Jimbo, Kata na Mtaa uliofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Arnatoglou Jijini Dar es Salaam .
Aidha, Ndg. Mabelya ameeleza kuwa mafunzo hayo ya siku (1) yamelenga kuhakikisha kwamba uchaguzi unafanyika kwa haki na ufanisi, huku yakiwaandaa wasimamizi wasaidizi na kuwapa ujuzi wa kutosha katika kusimamia mchakato wa uchaguzi kwa kuhakikisha kwamba kila hatua inatekelezwa kwa mujibu wa sheria, Kanuni na taratibu za uchaguzi.
"Kwa mamlaka niliyopewa na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya kifungu cha 201A cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka ya Miji) sura 288 kifungu cha 57(3) cha Sheria za Serikali za Mitaa pamoja na kanuni ya 7(1) ya uchaguzi wa viongozi wa mamlaka ya Serikali za Mitaa ngazi ya Vijiji, Vitongoji na Mitaa 2024 zilizotolewa kwa tangazo la Serikali namba 571,574 na 575 ya mwaka 2024 na Mwongozo wa Uchaguzi wa tarehe 09, Septemba 2024 vilivyotumika kwa ajili ya kuwateuwa kuwa Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivyo naamini baada ya mafunzo haya uchaguzi utafanyika kwa ufanisi mkubwa kwa kuzingatia sheria na kanuni za uchaguzi ili kuondoa malalamiko wakati wote wa uchaguzi."
Sambamba na hilo, Ndg.Mabelya amewataka washiriki hao kuzingatia mafunzo pamoja na kutoa uzoefu wao wa usimamizi wa siku za nyuma ili iwe rahisi katika utekelezaji wa jukumu zima la uchaguzi wa Serikali za Mitaa ifikapo Novemba 27, 2024 huku akiwakumbusha kuzingatia falsafa ya 4R (Reconciliation, Reform, Resilience na Rebuild) ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kifanikisha zoezi hilo kwa haki na uzalendo kwa maslahi ya Jiji na Nchi kwa ujumla.
Halikadhalika, Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi wamekula kiapo cha uaminifu, utii ,uadilifu na kutunza siri katika kutimiza majukumu yao na kuwatendea haki watu wote kwa mujibu wa sheria kanuni na taratibu za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.