Watahiniwa wapatao 21440,katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Tarehe 14 Novemba,2022 wameungana na maelfu ya watahiniwa wengine kote nchini kuanza kufanya mitihani yao ya kumaliza kidato cha nne.
Akitoa taarifa juu ya watahiniwa hao Mwl.Musa Ally ambaye ni Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam amesema kuwa wao kama walimu wamejiandaa vizuri katika kuwaandaa watahiniwa wao na wana matarajio makubwa juu yao kuwa watafanya vizuri kama ilivyo ada.
Aidha Mwl. Musa ametoa mchanganuo wa takwimu za watahiniwa hao na kusema kuwa katika watahiniwa 21440, wavulana ni 10969 na wasichana ni 10471. Pia kuna watahiniwa wa mitihani ya maarifa maarufu kama QT na wale wa mitihani ya kidato cha nne, ambapo watahiniwa wa mtihani wa Maarifa wapo 9971,watahiniwa wa kujitegemea ni 2164 na watahiniwa wa shuleni ni 18305.
Kwa upande wa watahiniwa walio na mahitaji maalum,amesema kuwa kuna jumla ya watahiniwa 43, ambapo 17 wapo katika shule ya Sekondari Jangwani, 25 wapo Pugu Sekondari na 1 yupo katika shule ya Sekondari Alhalamain.
Ameongeza kuwa watahiniwa hao wote wapo katika vituo 101 vya shuleni na vituo 8 vya watahiniwa wa kujitegemea.
Sambamba na Takwimu hizo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha sekta ya elimu nchini na kuhakikisha kunakuwa na mazingira salama ya Watoto kujifunzia.
“Ninamshukuru Mhe.Rais kwa namna anavyoendelea kuiwezesha sekta ya elimu kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI, ambapo wamekuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto mbalimbali na kuboresha miundombinu ya kutolea elimu nchini.” Amesema Mwl.Musa.
Akiongea kwa niaba ya wakuu wote wa shule za Sekondari zilizopo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Mwl.Joseph Deo ambaye ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Benjamini W.Mkapa amesema kuwa wao Kama Walimu wamewaandaa vizuri watoto hao sio tu kwa elimu ya darasani bali ya maisha pia,hivyo wana matarajio makubwa kuwa watafanya vizuri na ufaulu wao utakuwa wa juu kuliko mwaka uliopita.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.