Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Ndg. Jomaary Satura amewataka watumishi wa Jiji hilo kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wakati ili miradi hiyo iweze kutoa huduma kwa wananchi Kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Mkurugenzi Satura ameyasema hayo Machi 11, 2024 wakati wa kikao kilichowahusisha watumishi kutoka Idara za Elimu Msingi na Sekondari, Afya, Ugavi na Manunuzi pamoja na Ujenzi ambacho kililenga kujadili Utekelezaji wa Miradi.
Sambamba na hilo, Ndg. Satura ameongeza kuwa watumishi wa Jiji kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa, Wilaya pamoja na Mstahiki Meya wote wanawajibu wa kuboresha ustawi wa maisha ya wananchi wa Jiji la Dar es Salaam na Watanzania kwa ujumla, hivyo kwa watumishi wanaotamani kuendelea kufanya kazi katika Jiji hilo wametakiwa kuwa na utendaji kazi wa kiwango cha juu na yeyote atakayebainika kuihujumu Miradi inayotekelezwa na Serikali, hatua Kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
"Napenda kutoa rai kwa watumishi kufanya kazi kwa bidii na kutekeleza miradi kwa muda stahiki kwa maslahi ya wananchi, sisi tunapaswa kuwa Halmashauri ya mfano katika ukusanyaji wa mapato na utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo kwa sababu Halmashauri yetu ina idadi kubwa ya watumishi, idadi kubwa ya watu, pia ni kitovu cha uchumi wa cha Taifa na shughuli nyingi za Serikali zinazofanywa hapa kwetu hivyo tutambue jitihada za Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ambaye anapambana asubuhi na usiku kuhakikisha anapata fedha kwa ajili ya wananchi hivyo tuunge mkono juhudi vitendo." Amesema Ndg. Satura.
Aidha, ametoa pendekezo kwa Mstahiki Meya kuridhia kupunguza watumishi wa kada ya ugavi kutoka wafanyakazi 32 Hadi wafanyakazi 15, pia kada ya uhandisi kutoka wafanyakazi 44 Hadi 7.
Amesema ”Unapokuwa na watu wengi sana ufanisi na utendaji kazi unapungua, hivyo kupunguza wafanyakazi italeta ufanisi na uwajibikaji wa kazi, watumishi tutakao wapunguza nitawakabidhi wa Katibu Mkuu ambaye ninaamini ana upungufu wa watumishi katika mikoa ya pembezoni mwa Nchi.”
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyojitoa kuwahudumia wananchi na kutoa fedha za miradi ya maendeleo katika Jiji hilo.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Idara ya Manunuzi kushughulikia changamoto zote za mfumo wa Tausi zinazowakabili watumiaji wa mfumo huo ili miradi iliyopangwa kutekelezwa iweze kukamilika kwa wakati na kuwa chachu katika kuwaletea maendeleo wananchi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.