Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshiwa Selemani Jafo (Mb) leo tarehe 07 Mei, 2018 amefanya ziara ya kutembelea na kukagua eneo lenye hekari 12 ambalo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kujenga Kituo Kikuu cha kisasa cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Mbezi Luis.
Akiongea mbele ya viongozi wa Mkoa na Jiji la Dar es Salaam Mheshimiwa Jafo amesema Serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli imetoa fedha kiasi cha shilingi 146 bilioni kwa ajili ya miradi mkakati ya Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Jafo alieleza kwamba kati ya fedha hizo, shilingi 67.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa stendi za mabasi 6 na stendi 2 za malori ambapo Jiji la Dar es Salaam limetengewa kiasi cha shilingi 50 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani cha Mbezi Luis.
Katika hatua nyingine Waziri Jafo amewataka viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na busara wakati wa kutatua migogoro na ulipaji wa fidia kwa lengo la kuongeza eneo la ujenzi wa kituo hicho na pia kujenga miundombinu yenye ubora na inayozingatia mahitaji halisi ya wananchi hasa mamalishe, wamachinga na bodaboda na kuweza kukuza uchumi wa watu binafsi na taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Jafo alielekeza kwamba ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mbezi Luis unapaswa uwe wa mfano kwa kuzingatia kuwa Dar es Salaam ni Jiji la biashara na ujenzi wa kituo hicho unategemewa kupunguza msongamano jijini na miundombinu yake inapaswa kuwa rafiki na kufikika kirahisi na watumiaji wa Kituo jirani cha daladala cha Mbezi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana, alisema tathmini ya ulipaji wa fidia kwa wananchi imeshakamilika na hivi karibuni wananchi hao watalipwa stahiki zao na hadi tarehe 26 Juni, 2018 kazi ya ujenzi inatarajiwa kuanza baada ya Mkandarasi atakayeshinda zabuni kukabidhiwa eneo hilo la Mbezi Luis.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.