Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi (Mb.) leo tarehe 29 Novemba, 2018 jijini Dar es Salaam amefunga rasmi ofisi za Ardhi za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuagiza Maafisa Ardhi na Maafisa Mipangomiji wa Idara ya Mipangomiji, Mazingira na Usafirishaji katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wahamishiwe katika ofisi za Ardhi Kanda ya Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Bi. Sipora Liana, Maafisa Ardhi na Maafisa Mipangomiji wa Halmashauri za Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari, Waziri Lukuvi ameeleza kwamba kimuundo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam haina ardhi, haipimi ardhi, haipangi wala kumimilikisha ardhi hivyo majukumu hayo yanapaswa kufanyika katika Manispaa tano za Jiji la Dar es Salaam ambazo ni Manispaa za Ilala, Temeke, Kinondoni, Ubungo na Kigamboni.
Waziri Lukuvi aliendelea kueleza kwamba amefuta ofa zote zilizotolewa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuwataka wananchi wote wa Dar es Salaam wanaomiliki viwanja kwa ofa zilizotolewa na Halmashauri hiyo kwenda kuwaona Maafisa Ardhi wa Manispaa husika na kujitambulisha ili wapewe hati na kuepuka kutapeliwa.
Aidha, Waziri Lukuvi amempongeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa juhudi zake za kuhakikisha kwamba nyaraka zote za ardhi zilizopo katika ofisi yake zinahamishiwa katika Manispaa za Dar es Salaam na kumuagiza Kamishna wa ardhi Kanda ya Dar es Salaam kuzikagua ili kuwezesha zoezi la utoaji wa Hati za Kidigitali kwa Manispaa zote za Jiji la Dar es Salaam linaanza ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.