Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohammed Mchengerwa (Mb) amewataka viongozi wa Mikoa pamoja na Serikali za Mitaa kusimamia vizuri na kulinda maslahi ya Walimu na Watumishi wote Nchini wanaosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya kukabidhi vitendea kazi vipya ikiwemo Gari Toyota Coaster Mini Bus moja (1), Pikipiki 62 pamoja na Kompyuta mpakato 159 kwa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) iliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Tambaza Jijini Dar es Salam.
Akiongea wakati wa hafla hiyo Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa “Tunamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini kwani zaidi ya shilingi bilioni 800 zimetumika kwaajili ya elimu bure hivyo kwa kutambua juhudi hizo inabidi tufanye kazi kwa bidii kwa kuhakikisha tunasimamia vyema miradi ya elimu ikamilike kwa wakati sambamba na kuhakikisha maslahi ya walimu yanazingatiwa na kulindwa kwani ili tutoe elimu bora lazima tutengeneze mazingira bora kwa walimu kwa kuzingatia misingi aliyotuachia Baba wa Taifa ya kuhakikisha tunapambana na adui watatu yani umaskini, maradhi na ujinga hivyo niwaagize TSC kufanya Mapitio kwa walimu wote wanaostahili kupanda vyeo ili waweze kupanda kwa wakati.”
Sambamba na hilo Mhe. Mchengerwa amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia miradi yote inayotekelezwa katika Halmashauri zao ikiwemo ujenzi wa madarasa kukamilika kwa wakati na ikitokea hawajakamilisha hatua za kisheria zitachukuliwa huku akiendelea kuwasisitiza Wakurugenzi wa Halmashauri kupanga mipango ya maendeleo inayoendana na matumizi husika ambayo yanalenga wananchi hivyo vipaumbele vya maendeleo viwaguse wananchi moja kwa moja.
Awali Akitoa Shukrani zake kwa Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha sekta ya elimu nchini Mkuu wa Wilaya Mhe. Edward Mpogolo amesema “Kwa kipindi cha miaka miwili ya Rais wetu Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tumepokea zaidi ya bilioni 20 kwaajili ya kuboresha miundombinu ya elimu pamoja na kuendesha elimu bure ambapo nasisi kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri tumeweza kutengeneza madawati elfu 20 kwa Shule za Msingi pamoja na viti na meza 17,600 kwa shule za Sekondari za Halmashauri ya Jiji na utekelezaji unaendelea hivyo nikuhakikishie Mheshimiwa Waziri tutaendelea kusimamia yale yote utakayotuelekeza kwa maslahi ya Wananchi wetu na Nchi kwa ujumla.”
Kwa upande wake Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Paulina Nkwama ameeleza kuwa shilingi milioni 454.6 fedha kutoka mradi wa boost zimetumika kununua vitendea kazi vilivyokabidhiwa kwa watendaji wa TSC nchini ikiwemo Pikipiki 62, gari moja kwaajili ya kazi za makao makuu, pamoja na kompyuta mpakato 159 ambapo 139 zitagawanywa katika wilaya zote Nchini huku 20 zikibaki kwa matumizi ya Makao makuu, hivyo kutoa shukrani zake kwa Rais na kumuhakikishia mpaka 2025 sekta ya elimu nchini itakuwa imeboreshwa zaidi.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.