Historia ya jina Kariakoo na soko la Kariakoo inaanzia mwaka 1914 wakati nchi yetu Tanganyika ikitawaliwa na Wajerumani. Mahali palipo soko la Kariakoo palijengwa jengo na Wajerumani ambalo lilikua lifanywe ukumbi wa kuadhimishwa kutawazwa kwa mfalme Kaiser Wilheim wa Wajerumani lakini mara tu baada ya jengo kukamilika, vita kuu ya kwanza ilianza na Waingereza walipouteka mji huu wa Dar es Salaam walilitumia jengo hili kama kambi ya jeshi kwa askari walio julikana kama "Carrier corps” kwa jina la kigeni, yaani wabeba mizigo likitafsiriwa katika Kiswahili. Jina hilo la maaskari wabeba mizigo katika Kiswahili lilitamkwa kama “Karia-koo” na liliendelea kutumika kama jina la eneo lote linalozunguka mahali pale hii ndio historia ya jina Kariakoo.
Baada ya vita kuu ya kwanza kwisha, mwaka 1919 na nchi yetu kuanza kutawaliwa na Waingereza jengo hili lilianza kutumika kama soko na kuanza kuhudumia wakazi wa mji huu.
Wakati huo wafanya biashara walikua wakiuza bidhaa zao sakafuni kwa sababu hapakua na meza. Wafanyabiashara waliendelea kufanya biashara sakafuni hadi miaka ya 1960 wakati meza za saruji zilipo jengwa. Kwa kadri Jiji la Dar es Salaam lilivokua na wakazi wake kuongezeka, ndivyo kadri Soko hilo la zamani lilivyokua likishindwa kumudu kutoa huduma nzuri kwa wananchi. Pamoja na kubanana katika soko hilo na biashara kufanyika katika mazingira yasiyo ridhisha, pia halikua na ghala za kutunzia vyakula wala vyumba vya barafu vya kuhifadhia vyakula. Hali hiyo iliwafanya viongozi wa Halmashauri ya Jiji kuona haja ya kuwa na soko kubwa na la kisasa kulingana na maendeleo ya Jiji na hivyo wakaanza kujadili uwezekano wakujenga Soko jipya.
Uamuzi wakujenga soko kuu la Kariakoo la sasa, ulifanywa na Serikali mnamo mwaka 1970 baada ya majadiliano yaliyo chukua muda mrefu kati ya vyombo vya Serikali vilivyohusika. Serikali iliagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kufanya mipango ya ujenzi wa soko jipya la kisasa ambalo lingechukua nafasi ya soko la zamani lililokua hapa Kariakoo. Matarajio ya uamuzi huu wa Serikali wa kujenga Soko jipya yalikua ni kuwapatia wakazi wa Jiji mahala au Soko kubwa ambalo lingetosheleza mahitaji yao kwa muda wa miaka 50 hadi 70 ijayo kuhusu mambo yote ya vyakula, yaani uuzaji jumla, mahala pakuhifadhi vyakula na uuzaji wa rejareja. Mipango yote ilikamilika na ujenzi ulianza rasmi mwezi Machi, 1971. Ramani ya jengo la Soko ilitayarishwa na mchoraji wa ramani za majengo hayati Beda J. Amuli ambaye ni mtanzania aliyeishi Dar es Salaam. Wajenzi waliojenga jengo la Soko ni Mwananchi Engeneering and Contracting Company (Mecco) wakisaidiana na makontrakta wengine kadhaa kwa kazi mbalimbali zilizo hitaji wataalamu maalumu. Shughuli zote za ujenzi zilimalizika mwezi Novemba 1975, na Soko lilifunguliwa rasmi kwa matumizi ya wananchi hapo tarehe 8 Desemba, 1975 na hayati Mwalimu Julius K.Nyerere, Raisi wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mpaka kukamilika, ujenzi wa Soko uligharimu jumla ya shilingi 22 milioni.
Soko la Kariakoo lipo kati kati ya eneo la Kariakoo katika kiwanja namba 32 zone 111 na limezungukwa na mitaa ya Nyamwezi, Mkunguni, Sikukuu na Tandamti.
Soko lina majengo mawili ambayo yameunganishwa katika ghorofa ya chini ya ardhi. Majengo haya mawili pamoja na sehemu inayounganishwa yana eneo lenye jumla ya mita za mraba 17,780. Jengo la kwanza linaweza kuitwa Soko kubwa na jengo la pilli Soko dogo. Soko kubwa limegawanyika sehemu tatu ambazo ni ghorofa ya kwanza, ghorofa ya katikati, na ghorofa ya chini ambayo ni (basement). Soko dogo ni la rejareja ambalo ni tofauti sana na masoko mengine ya Dar es Salaam.
Shirika la masoko Kariakoo lilianzishwa kwa mujibu wa sheria ya Bunge Na.36 ya mwaka 1974. Mnamo mwaka 1985, sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho kwa kurekebisha kifungu Namba 8 cha sheria hiyo. Katika marekebisho hayo Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam lilimilikishwa asilimia 51 ya hisa na Msajili wa Hazina akabaki na hisa asilimia 49. Sheria ya Shirika la masoko ya Kariakoo pia imefanyiwa marejeo mwaka 2002 (Revised edition) na kutambulika kama (The Kariakoo Makert Corporation revised Edition Act. No.132 of 2002 na kupewa majukumu yake makuu yafuatayo;
2.0 DIRA (VISION)
Dira ya Shirika ya Masoko ya Kariakoo kuwa Soko la kisasa katika Nchi za Afrika Mashariki na ya kati kwa kutoa huduma nzuri na endelevu hususani mazao ya vyakula, pembejeo za kilimo na Bidhaa mchanganyiko zenye kujali Afya, mazingira na usalama wa watumiaji / walaji (consumers).
2.1 DHAMIRA (MISSION)
Kutumia aina zote za rasilimali zilizopo na kuwashirikisha wadau mbalibmali katika kujenga uwezo endelevu na ushindani katika Soko la kibiashara linalikidhi haja za wadau, kudhibiti ubora wa bidhaa, mawasiliano na usafirishaji kwa ujumla .
2.2 TUNU ZA MSINGI (CORE VALUES)
Shirika la masoko Kariakoo linaamini yafuatayo katika utekelezaji wa shughuli zake
i.Hadhi na uwazi (Intergrity and transparency)
ii.Ushirikiano kazini (Teamwork)
iii.Kujituma na kuwajibika (commitment and accountability)
iv.Huduma bora (quality services)
v.Weledi (professionalism)
vi.Uwajibikaji kwa jamii (social responsibility)
3.0 UTAWALA/UONGOZI
Shirika la Masoko ya Kariakoo lipo chini ya Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Shirika lina wanahisa (2) ambao ni Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo ina HISA 51% na HAZINA inayomiliki 49%.
(a) Bodi ya Wakurugenzi
Kwa mujibu wa sheria, Shirika linatakiwa kusimamiwa na Bodi ya Wakurugenzi. Ambapo Mwenyekiti wa Bodi huteuliwa na Mheshimiwa Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wajumbe wa Bodi huteuliwa na Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(OR-TAMISEMI).
(b) Menejimenti.
Chini ya Bodi iko Menejimenti inayoongozwa na Meneja Mkuu ambaye huteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ndiye Msimamizi Mkuu wa uendeshaji wa shuguli za kila siku za Shirika.
Shirika lina Idara nne (4) na Vitengo sita (6).
Soko la Kariakoo
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.