Sekta ya viwanda ni miongoni mwa sekta zinazochangia pato la taifa, sekta hii inatoa ajira kwa watanzania wengi wanaofanyakazi katka viwanda vidogo na vya kati.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika kutekeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya kukuza uchumi wa nchi yetu katika maendeleo ya sekta za viwanda, biashara, masoko, viwanda vidogo, biashara ndogo na uwekezaji imeanza ujenzi wa miundombinu, majengo na maeneo ya huduma kwa ajili ya wajasiriamali wadogo kwa kushirikiana na Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO).
Lengo la ujenzi wa viwanda hivi vidogo ni kuwafikishia huduma muhimu wanawake na vijana kwa pamoja ili wajikwamue kiuchumi, kujiongeza kipato na kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana na kina mama kwa kuwarasimisha wajasiriamali hawa wadogo ambao wengi hawako rasmi kwa kukosa sehemu za kufanyia kazi.
Awamu ya kwanza mradi huo utahusisha ujenzi wa majengo makubwa mawili yenye vyumba vitatu kila kimoja kwa ajili ya biashara umepangwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 190, hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai, 2017 utakuwa umekamilika kwa asilimia 82.
Hadi kufikia mwezi Agosti, 2017 ujenzi wa miundombinu hiyo umefikia asilimia 95. Gharama za mradi huo ni shilingi 199,988,052.00. Ujenzi huo utaendelea kutekelezwa na Halmashauri ya Jiji katika Manispaa za Ilala, Kigamboni, Temeke na Ubungo kwa kadri maeneo yatakavyopatikana.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ambayo inashirikiana na Shirika la Kukuza Viwanda Vidogo Vidogo(SIDO) kuwajengea uwezo wajasiriamali hao itawawezesha kupata mafunzo yatakayowasaidia kuboresha zaidi uzalishaji na biashara zao. Kwa upande mwingine itakuwa rahisi zaidi kwao kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha, wadau mbalimbali pamoja na huduma muhimu kutoka Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) na wadau wengine.
Ujenzi huu utagharimu takribani Tsh.400 Milioni zikihusisha ujenzi wa maduka saba (7) ya kukodisha pamoja na vyoo vya matundu 10 na baada ya kukamilika Viwanda hivi vinatarajia kutoa ajira kwa wastani wa watu 300.
Kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi, tovuti ya Halmashauri pamoja na mitandao ya kijami, Halmashauri ya Jiji itawasaidia wajasiriamali hao kujitangaza zaidi ili waweze kupata masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi na inatoa wito kwa wajasiriamali wote watakaopata nafasi katika viwanda hivyo kuitunza miundombinu katika maeneo yote yatakayojengwa viwanda hivyo kwa maslahi ya wananchi wote.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Anuani ya Posta: S.L.P 20950
Simu ya mezani: 0738 378 386
Namba ya Mkononi: 0738 378 386
Barua Pepe: info@dcc.go.tz
Hatimiliki © 2017 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Haki Zote Zimehifadhiwa.