Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Ng’wilabuzu Ludigija leo tarehe 13 Julai, 2022 amefanya ziara ya kukagua ukarabati na ujenzi wa Soko Kuu la Kariakoo, kwa lengo la kuona namna hatua za ujenzi huo unavyoendelea sambamba na matarajio ya kukamilika kwa mradi huo. Ukarabati wa soko hilo umetokana na ajali ya moto iliyotokea miezi kadhaa iliyopita na kusababisha hasara kwa kuteketeza mali zilizopo.
Aidha, ukarabati huo unaenda sambamba na ujenzi wa Soko Dogo lililopo pembeni ya Soko Kuu la Kariakoo. Akiongea katika ziara hiyo Mhe. Ludigija amesema “Namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa, Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha ambazo zinatumika katika ujenzi wa soko dogo na ukarabati wa soko kuu la kariakoo, shilingi Bilioni 28 Rais wetu amezitoa kukamilisha ujenzi huu, ikiwa Bilioni 26 kwa ajili ya Mkandarasi na Shiling Bilioni 2 kwa ajili ya Mshauri wa Ujenzi huu ambao ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), hii inaonesha namna Rais anajali wafanya biashara katika soko hili”.
Katika ziara hiyo Mhe. Ludigija aliambatana na wafanyabiashara pamoja na viongozi wa Soko Dogo na Soko Kubwa la Kariakoo na viongozi wa wamachinga kwa madhumuni ya kuja kuangalia ujenzi unavyoendelea na kuzidi kuwa na imani na Serikali juu wafanyabiashara wote kurejea pindi soko litakapomalizika.
“Napenda kuwahakikishia kwamba wafanyabiashara wote kuwa na usawa katika biashara kutokana na ukweli kwamba kuna wafanyabiashara wengi wamepisha ujenzi pamoja na ukarabati huu, hivyo basi wote muwe na subira na mtakuwa kipaumbele cha kwanza kurudi katika soko hili kama mwanzo ili mfanye biashara zenu bila ya wasiwasi”.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, alitoa wito kwa wafanyabiashara wadogowadogo maarufu kama Machinga kuacha mara moja kurudi katika maeneo ambayo siyo rasmi kwa wafanyabiashara na kuwasihii watengezaji wa simu za mkononi kutozuia Barabara za watembea kwa miguu.
Ujenzi na ukarabati wa soko kuu la Kariakoo mpaka sasa umefikia asilimia 28% ya ujenzi ikiwa unatarajiwa kumalizika mnamo Agosti, 2023 akieleza Mkandarasi wa Ujenzi huo Ndugu, Johnson Nyamwelu, amesema “katika nafasi yetu kama wakandarasi kwanza tunaunga mkono Serikali ya awamu ya Sita sambamba na kusimamia ujenzi huu ambao kwa sasa unaenda vizuri malengo yetu kumaliza kabla ya wakati ili kumheshimisha Rais wetu kwa utekelezaji bora wa ujenzi huu”
Ukarabati wa Soko Kuu la Kariakoo unatarajiwa kuboreshwa zaidi ukitofautisha na ulivyokuwa awali ikiwa maboresho zaidi katika kuongeza sehemu za biashara za mabenki, uwekwaji wa lifti, kuongeza maeneo zaidi ya wafanya biashara wadogo na wakubwa ikiwa ni dhamira ya kuweza kuwarudisha wote waliopisha ujenzi na ukarabati kurudi na kuendelea kufanya biashara kama awali.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa Mkuu wa Wilaya kuweza kutembelea Soko Kuu la Kisutu na kuweza kuongea na wafanyabiashara wa soko hilo ili kusikia kero zao pamoja na kutafuta njia ya upatikanaji wa suluhisho, sambamba na kuwsikiliza wafanya biashara katika soko dogo la Uuzaji wa Kuku.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.