Katika kuendeleza na kutekeleza kampeni ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla, Mkuu wa Wilaya ya Ilala Leo Machi 25,2023 ameshiriki zoezi la usafi katika Kata ya Kipawa, ambao usafi huo ulijumuisha maeneo ya Barabara ya Air Port, Maeneo ya Kata ya Kiwalani, Vingunguti na Minazi Mirefu hadi kufika daraja la Mfugale.
Zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo akiambatana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala , Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Diwani wa Kata ya Kipawa , Diwani wa Viti Maalumu, Watumishi Kutoka Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Watendaji wa Mtaa, viongozi wa Chama cha Mapinduzi ,viongozi kutoka shujaa wa maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA),wadau kutoka Bank ya CRDB na NMB, wadau mbali mbali wa usafi wakiwemo Wejisa Company limited , Kajenjere Trading Company Limited, Sateki Trading Limited, pamoja na Wananchi wa Kata ya Kiwalani,Minazi Mirefu Kipawa na Vingunguti.
Akiongoza Mhe. Edward Mpogolo amewashukuru viongozi wa Serikali za mitaa na Kata kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi huu kwani wameonesha kuwiwa na jambo hili.
“Kutokana na ukubwa wa Barabara ya Airport napenda kuwaomba watu wa maduka na Makampuni yaliyoko barabarani waboreshe maeneo Yao huku upande wa katika ya barabara tutahakikisha Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam tunashirikiana na wadau mbali mbali ili kuhakikisha barabara hii inakuaje safi na bora kwani Dar es Salaam hususani Wilaya ya Ilala Ndio Kitovu cha kupokea wageni wanaoingia Nchini kwani hivi karibuni tutakua na ugeni mkubwa Nchini kwetu ambapo tutampokea Makamu wa Rais wa Marekani Mhe. Kamala Harris hivyo tuweke mazingira yetu katika hali ya usafi wakati wote ili pindi wageni wetu hao wanapofika wajivunie mazingira ya Nchi yetu yanavyopendeza na kuvutia yakiwa katika hali ya usafi .”
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo amemuelekeza Mkurugenzi wa Jiji kwa kushirikiana na watendaji wake kuhakikisha wanaenda barua na kuwapelekea wafanyabiashara wote wenye Majengo kuanzia barabara ya Airport hadi Ikulu ili kuona namna gani watawaelekeza kuboresha mazingira na miti gani waweze kupanda kwenye maeneo Yao ili kuboresha mazingira ya Mji wetu.
Aidha Mhe. Mpogolo amewataka watu wa viwanda na makampuni yaliyoko barabarani kuhakikisha wanafanya usafi mara kwa mara katika maeneo yao na kupanda miti inayokubalika.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Bi.Tabu Shaibu ameeleza kuwa kampeni hii ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam imekua ya mafanikio zaidi kwa Jiji la Dar es Salaam kuwa Safi kwani wananchi wameonekana kujitokeza kwa wingi katika zoezi la usafi.
“Nipende kutoa Shukrani zangu za dhati kwa Mkuu wa Mkoa Wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla kwa kuanzisha Kampeni hii ambayo ni endelevu hivyo niwaombe wananchi kuhakikisha usafi ni Sehemu ya maisha yetu ya Kila siku na si mpaka tusubiri usafi wa mwisho wa mwezi.” Ameeleza Bi. Tabu Shaibu.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.