Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo amewataka Waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanasimamia vyema utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo kwa ukaribu zaidi ili ikamilike kwa wakati, hayo ameyasema leo Oktoba 19, 2023 Katika Ukumbi wa Arnatouglou Jijini Dar es Salaam wakati wa kikao maalumu cha Madiwani kupitisha taarifa ya ujenzi wa masoko ya kisasa.
Akizungumza katika kikao hicho Mhe. Mpogolo amesema “Lengo la kikao hichi ni kuwaasilisha michoro ya majengo ya Masoko ya kisasa yanayoenda kutekelezwa katika Halmashauri yetu ikiwemo Soko la Ilala na Mchikichini ambayo yatakwenda kutuongezea mapato zaidi yatakayo tumika kuendeleza sekta nyingine za Afya pamoja na Elimu ikiwa ni kutekeleza adhima ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha miundombinu na kuwapanga wafanyabiashara kufanya biashara katika maeneo maalumu hivyo niwaombe Waheshimiwa Madiwani kwa kushirikiana na viongozi wa Jiji la DSM msimamie miradi hii iweze kukamilika kwa wakati kwani jitihada za kuongeza mapato ndio zimeleta miradi hii ya kimkakati kwakua ujenzi wa Masoko haya utatusaidia kuwatambua wafanyabiashara na kudhibiti upotevu wa mapato.”
Sambamba na hilo Mhe. Mpogolo amewataka viongozi hao kushirikiana na kuwataka Waheshimiwa Madiwani kuainisha maeneo ya wazi yanayopatikana kwenye Kata zao kwani kupitia maeneo hayo miradi mingi itaendelea kutekelezwa kwa Kasi zaidi.
Kwa Upande wake Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto amemuhakikishia Mkuu wa Wilaya ya Ilala kutekeleza yote aliyoelekeza huku akimuahidi kuwa atashirikiana na Kamati zake za kudumu za Halmashauri kusimamia miradi hiyo ipasavyo ili ikamilike kwa wakati ikiwa ni sehemu ya kuboresha miundombinu pamoja na utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salam Bw. Jomaary Satura ameeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwashirikisha Madiwani katika utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati ili waweze kutoa maoni kwani anaamini kupitia miradi hiyo Halmashauri itaenda kukusanya mapato kwa wingi na kupita lengo hata hivyo baada ya kuanzishwa Kanda saba za Huduma Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam robo ya Kwanza (Julai hadi Septemba) imeweza kukusanya kiasi cha shilingi bilion 31.5 hii inaonesha ni jinsi gani Jiji la Dar es Salaam limejikita katika kukusanya mapato na kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa ukaribu zaidi.
Aidha, katika kikao hicho wajumbe waliweza kufundishwa jinsi ya kuboresha na kupendezesha Mandhari ya Jiji la Dar es Salaam, namna ya kuitangaza Halmashauri katika utalii wa ndani, kuboresha eneo la Mnazi Mmoja kuwa la maegesho ya magari pamoja na kutenga eneo kwa ajili ya bandari kavu kwani kupitia miradi hii mapato ya Halmashauri yatazidi kuongezeka kwa kiwango kikubwa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.