Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mheshimiwa Edward Mpogolo amefungua mafunzo kwa viongozi kuhusu mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Jiji huku akitoa wito kwa Madiwani kuhakikisha mikopo hiyo inawanufaisha walengwa.
Mafunzo hayo yaliyoambatana na kula kiapo kwa timu ya Menejimenti, Kamati ya huduma ya Mikopo na Kamati ya uhakiki ngazi ya Wilaya yaliyofanyika Novemba 25, 2024 yamewakutanisha Madiwani wa Kata zote 36 za Wilaya hii pamoja na Menejimenti ya Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam.
Mkuu huyo wa Wilaya, amewataka Viongozi hao kutojihusisha na upendeleo katika kusimamia zoezi la utoaji wa mikopo hiyo huku akiwakumbusha kuweka mbele maslahi ya Nchi.
"Ninyi wote ni mashahidi kwa mikopo ile ya awali mambo mengi yalijitokeza, niwaombe nendeni mkasimamie mikopo hii ili iweze kuwafikia walengwa". Alisisitiza Mhe. Mpogolo
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kurejesha mikopo hiyo kwa vikundi vya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu ambayo inawapa fursa wale ambao hawana uwezo wa kukopa katika Taasisi za kifedha.
Aidha, Mkurugenzi Mabelya alibainisha kuwa Halmashauri ya Jiji imetenga kiasi cha Shilingi bilioni 14.85 kuwezesha utoaji wa mikopo hiyo kwa vikundi ambavyo tayari vimeshafuata taratibu.
Ikumbukwe kuwa hivi karibuni vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu vikiwa na wajasiriamali zaidi ya elfu 4 walikutana katika kongamano kubwa lililofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja lililokuwa na lengo la kutoa elimu kuhusu mikopo hiyo.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.