Na: Doina Mwambagi
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Edward Mpogolo, amezitaka taasisi za kifedha kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanufaika wanapata mkopo kwa wakati.
Hayo ameyasema Leo februari 24, 2025 kwenye mkutano maalumu wa utambulisho wa benki katika usimamizi na utaoji wa mikopo halmashauri ya Jiji uliofanyika katika ukumbi wa Anartoglo Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Mpogolo amesema dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha ,wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapata mikopo ili kuwakwamua kiuchumi
“Serikali inaamini kwamba uwezeshaji wa makundi haya utaongeza usawa na kuboresha hali ya maisha yao. Mikopo hii inalenga kuwawezesha kupata fursa za kiuchumi ambazo zitawawezesha kujitegemea na kuchangia katika maendeleo ya taifa. Hivyo nitoe wito kwa benki ya CRDB na NMB kuhakikisha wanufaika hao wanapata mikopo yao kwa wakati, ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi.' Amesisitiza Mhe. Mpogolo.
Aidha, DC Mpogolo ameziagiza taasisi za kifedha kutengeneza mfumo mzuri wa ufuatiliaji wa madeni ili kuhakikisha kuwa wanufaika wanarejesha mikopo yao kwa wakati na kwa njia inayohusisha uwazi na usimamizi mzuri pia utasaidia katika utunzaji wa rekodi za kifedha kwa faida ya wateja
Sambamba na hilo, Mhe. Mpogolo amesema kwa kuunga juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika matumizi ya nishati safi ya kupikia amezitaka benki hizo kutoa mikopo ya majiko ya kisasa kwa mama lishe na baba lishe ili kulinda afya zao na mazingira kiujumla.
Lengo kuu la mkutano huu lilikuwa ni kutambulisha benki ya CRDB na NMB zitakazoshirikiana na halmashauri katika kusimamia utoaji wa mikopo.
Serikali iliisimamisha mikopo hiyo ya 10% ili kufanya maboresho, na sasa imechagua Halmashauri 10 za mfano, ikiwemo Jiji la Dar es Salaam na tayari imeingia makubaliano na benki mbili ya CRDB na benki ya NMB kwa ajili ya utoaji wa mikopo hiyo, huku shilingi bilioni 15 zikiwa zimetengwa kwa ajili ya Mikopo kutoka kwenye mapato ya ndani na marejesho ya mikopo ya awali. Hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa wanufaika wanapata fursa bora zaidi za mikopo kwa maendeleo yao.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.