Na: Rosetha Gange
Wakati wataalamu wa afya dunia wakiendelea kuumiza vichwa juu ya tiba ya kulimaliza kabisa janga la UVIKO 19, hapa kwetu Tanzania Serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zimekuwa zikiungana na wataalamu hao duniani kote katika kupunguza maambukizi ya ugonjwa huo ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu kupata chanjo, kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima, kuvaa barakoa wawapo kwenye mikusanyiko, kutumia vitakasa mikono na kunawa mikono kwa maji tiririka mara kwa mara.
Katika kuunga mkono jitihata zinazofanywa na Serikali ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania,Shirika la Dar es salaam Hamburg Partnership linalomilikiwa na watu wa Ujerumani hapa Tanzania limegawa vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi ya UVIKO 19 katika shule mbalimbali za watoto wenye mahitaji maalumu katika mkoa la Dar es salaam pamoja na kutoa elimu kwa watoto hao ya namna ya kutumia vifaa hivyo na njia nyingine za kujikinga na virusi vya Uviko 19.
Zoezi la ugawaji wa vifaa hivyo ulianza tarehe 4/10 na kumalizika 12/10/2021. Vifaa vilivyogawiwa ni Pamoja na stendi za chuma kwa ajili ya kuwekea ndoo za maji, ndoo za kutunzia maji na bomba zake, sabuni za maji za kunawia mikono pamoja na barakoa.
Akikabidhi vifaa hivyo Dr. Sylivia Ruambo ambaye ndiye Mratibu wa zoezi hilo amesema “Kama tunavyojua janga hili la UVIKO 19 lipo na tunapaswa kujikinga nalo sababu halichagui mtu mzima wala mlemavu.Tumeamua kuwasaidia Watoto wenye ulemavu kwa namna ya pekee kwa sababu changamoto wanazozipata wengine sababu ya ugonjwa huu na wao wanazipata lakini wao kutokana na hali walizonazo changamoto hizo huwa kubwa zaidi. Hivyo njia za kuwakinga kirahisi ni kuwawekea mashine za kunawia mikono karibu ili kuwarahisishia walimu na walezi wao waweze kuwasaidia kirahisi”
Shule zilizokabidhiwa msaada wa vifaa hivyo ni Pamoja na Shule ya Sekondari Pugu, Shule ya msingi Mzambarauni, Shule ya msingi Buguruni Viziwi, shule ya Msingi Msimbazi Mseto,Shule ya sekondari Benjamini Mkapa,Shule ya msingi Uhuru mchanganyiko, Shule ya Sekondari ya wasichana Jangwani,Shule ya msingi Mtoni Maalumu, Shule ya msingi Sinza maalumu na Shule ya msingi Msasani.
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam, Afisa Elimu Maalumu wa Jiji Ndg.Swalehe Msechu ameishukuru Taasisi hiyo kwa kuwakumbuka watoto wenye changamoto mbalimbali kwani katika jamii mara nyingi kundi hili huwa linasahaulika sana. Hivyo kuwapa elimu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya UVIKO 19 kutawaepusha wao wenyewe na familia zao katika hatari ya kupata maradhi hayo.Pia ameahidi kusimamia utunzaji wa vifaa vyote vilivyokabidhiwa ili viweze kutumika katika matumizi sahihi yaliyokusudiwa.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.