Fursa za uwekezaji nchini zinaendelea kufungua milango na kuwavutia wawekezaji kutoka nchini China kuanzisha uhusiano na Jiji la Dar es Salaam kwa lengo la kuwekeza, kufanya biashara na kazi za ujenzi miundombinu mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam.
Naibu Meya wa Jiji la Liuzhou, Mheshimiwa Liu Ke, ambaye ametembelea Tanzania akiongoza ujumbe wa watu saba ambao ni wafanyabiashara na maafisa wa Halmashauri ya Jiji la Liuzhou, ameieleza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwamba Tanzania ina fursa nyingi katika sekta ya biashara na ujenzi, hususan katika Jiji la Dar es Salaam, ambazo wafanyabiashara na wananchi wa Liuzhou ingependa kuzitumia kwa kuwekeza na kufanya kazi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu kama barabara, reli, majengo ya aina mbalimbali na kutoa misaada itakayohitaji katika Jiji la Dar es Salaam.
Ameeleza kwamba Jiji la Liuzhou ambalo lina wakazi milioni nne limepiga hatua kubwa ya maendeleo katika sekta mbalimbali hasa biashara, viwanda vya magari na utengenezaji wa chuma. Kutokana na teknolojia kubwa waliyonayo, Naibu Meya huyo amesema kwamba kwa sasa Liuzhou inafanya maandalizi ya kutengeneza magari yatakayotumika bila kuwa na madereva baada ya kufanikiwa kutumia nishati ya umeme kwa uendeshaji wa magari yao.
Mheshimiwa Liu Ke alitumia fursa ya ziara yake Dar es Salaam kujikumbusha historia ya uhusiano ulioimarika kati ya China na Tanzania akirejea kumbukumbu za ujenzi wa reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA). Kiongozi huyo amemkaribisha Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita na ujumbe wake kutembelea Jiji la Liuzhou kukamilisha taratibu za kuanzisha Uhusiano wa Miji Dada kati ya Dar es Salaam na Liuzhou.
Kwa niaba ya Halmashauri ya Jiji na wakazi wa Dar es Salaam, Mstahiki Meya wa Jiji, Isaya Mwita, alimuhakikishia Naibu Meya huyo kwamba kutokana na urafiki wa kudumu wa Tanzania na China ulioasisiwa katika misingi ya urafiki wa dhati, Dar es Salaam ipo tayari kushirikiana na Liuzhou na kukubali miji hiyo kuwa na Uhusiano wa Miji Dada.
Mstahiki Meya Mwita amekubali kuongoza ujumbe wa viongozi wa Halmashauri za Mkoa wa Dar es Salaam kutembelea Jiji la Liuzhou. “Wananchi wa China na sisi Watanzania tumetofautia rangi tu, lakini roho zetu zimejaa upendo wa dhati unaoimarisha urafiki wa Tanzania na China,” alisema Mstahiki Meya Mwita alipokuwa akiukubali mwaliko wa kutembelea Jiji la Liuzhou.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.