Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepata hati safi kupitia taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali “CAG” kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa mara baada ya kumalizika kwa Kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kilichokuwa na ajenda moja ya kuwasilisha taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali “CAG", Mstahiki Meya Isaya Mwita alisema kuwa hati hiyo imetokana na kuwepo kwa usimamizi mzuri wa matumuzi ya fedha za Serikali.
Alifafanua kuwa kwa kiasi kikubwa tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo, ameendelea kusimamia na kupunguza matumizi ya fedha ambayo hayakuwa ya lazima jambo ambalo limeleta heshima kubwa katika Halmashauri hiyo.
Aliongeza kuwa mbali na hiyo, lakini pia kwa kiasi kikubwa mapato ya Jiji yameongezeka kutokana na kusimamia kikamilifu vyanzo vya mapato yaliyopo ndani ya Jiji.
Alifafanua kuwa hati hiyo inaleta heshima kubwa ndani ya Jiji na kwamba imetoa nafasi kwa watendaji ndani ya Halmashauri kufanya kazi kwa umahiri zaidi ili kuweza kuleta maendeleo makubwa kwa wananchi. Alisema taarifa ya CAG imeeleza wazi kuwa hali ya utekelezaji ndani ya Jiji ni ya kuridhisha kutokana na usimamizi wa kutosha, kufuatilia mambo na hivyo kuweza kuyafanyia kazi mapendekezo ya ukaguzi wa miaka ya nyuma yaliyosalia.
"Baada ya kupata hati hii, sasa ni wakati mwingine Jiji kuendelea kufanya kazi za kuwatumikia wananchi ili waweze kunufaika na rasilimali zao, ukiangalia tumepewa dhamana kubwa ya kuwatumikia, hivyo kama Meya mwenye Jiji sina budi kuwatumikia wananchi kama inavyotakiwa” alisema Meya Mwita.
Aidha Meya Mwita alitoa wito kwa Halmashauri zilizopo ndani ya Jiji la Dar es Salaam kuwatumikia wananchi ikiwemo kutatua kero zinazo wakabili.
Wakati huo huo, Meya Mwita alisema kuwa Jiji limetenga Shilingi milioni 500 kwa ajili ya kununua maeneo ya makaburi kutokana na kuwepo kwa changamoto ya maeneo ya kuzikia watu. Alisema kwa sasa hali imekuwa mbaya kwenye maeneo ya Jiji na kwamba pesa hizo zitatumika kununua maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya kuzikia watu wanapopoteza maisha.
"Jambo hili litaanza kufanyika mwaka huu, kila Halmashauri itapatiwa eneo kwa ajili ya kuzikia watu, yapo maeneo ambayo tumepanga kuyanunua ukiangalia Jiji letu lina watu wengi sana, kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo watu wanavyozidi kuongezeka. Leo hii imefikia hatua mtu ana zikwa juu ya mtu mwingine, jambo hili sio zuri” alisema Meya Mwita.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.