Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Dar es Salaam Ndugu Abbas Mtemvu ameushukuru Ubalozi wa China nchini Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuinua sekta ya Elimu nchini.
Mtemvu ameyasema hayo wakati wa Hafla ya kukabidhi viti na meza 80 vyenye thamani ya shilingi Mil.7.3 zilizogawiwa katika shule za Msingi na Sekondari za Jimbo la Ilala pamoja na vifaa vya michezo vilivyogharimu shilingi Mil.24 vilivyotolewa na Serikali ya watu wa China kupitia kwa balozi wake Chen Mingjian iliyofanyika tarehe 20 Machi 2024 katika viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilala ambaye pia Ni Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema kuwa vifaa hivyo walivyokabidhiwa ni namna mojawapo ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta ya Elimu na michezo nchini na kuongeza kuwa misaada hiyo sio tu itaimarisha ushirikiano baina ya Jimbo la Ilala na Ubalozi wa China bali na Serikali ya Tanzania na China.
Awali akiongea katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Edward Mpogolo ameeleza kuwa “Nipende kuwashukuru wenzetu kutoka Serikali ya China kupitia ubalozi wa China Nchini Tanzania kwa kuendelea kushirikiana nasi katika kuhakikisha uboreshaji wa elimu kwenye Jiji letu la Dar es Salaam hadi kutoa viti na meza 80 kwa Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari. Hivyo tunaahidi kushirikiana na wenzetu wa China katika kuhakikisha tunakuza Sekta ya Elimu nchini kwa kuwapatia Wanafunzi elimu bora pamoja na kutengeza mazingira rafiki ya kufundishia pia nitoe wito kwa Walimu waliokabidhiwa viti na meza hizi kuhakikisha wana vitunza ili viweze kudumu kwa muda mrefu”.
Naye Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema kuwa Serikali ya China itaendeleza urafiki na ushirikiano mzuri baina ya Jimbo la Ilala na Tanzania kwa ujumla kwa kuboresha maisha ya Watanzania na maendeleo ya vijana.
Aidha, viti na meza hizo zitagawanywa katika Shule 16 za Jimbo la Ilala zikiwemo shule 8 za Msingi na 8 za Sekondari huku vifaa vya michezo vikipelekwa katika Kata za Jimbo la Ilala kwaajili ya mashindano ya Ilala Super Cup.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.