Na: Hashim Jumbe
BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Tarehe 08 Februari, 2022 limefanya Mkutano Maalum wa Mapitio na Bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai-Desemba, 2021) na kufanya Makisio ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 wenye Jumla ya Shilingi Bilioni 193.8, ambapo kati ya fedha hizo Shilingi Bilioni 73.9 sawa na 38.1% ya Bajeti yote ni kutoka kwenye vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri na Shilingi Bilioni 119.9 sawa na 61.85% ya Bajeti ni fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya kawaida.
Aidha, kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto, kilipokea, kikajadili na kisha kupitisha Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo Bajeti ya Mapato ya ndani ya Halmashauri ya mwaka wa fedha 2022/2023 imeongezeka kwa 16% ukilinganisha na Bajeti ya Shilingi Bilioni 62 ya mwaka 2021/2022, hii imetokana na mikakati bora iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye ukusanyaji wa mapato.
Katika kuandaa Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imezingatia Muongozo wa uandaaji wa Bajeti uliotolewa na Hazina Mwezi Februari, 2021, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya Mwaka 2020, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa Bungeni.
Sambamba na hayo, lakini pia uandaaji wa Mpango na Bajeti umezingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 sura 439 pamoja na kanuni zake, Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya rushwa, Malengo ya Mellania (SDGs 2030) Mpango Mkakati wa Halmashauri, Maoni ya wadau mbalimbali wa Halmashauri ambao wameshiriki katika maandalizi ya bajeti hii kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata, Idara hadi Halmashauri kwa ujumla kwa kutumia mfumo wa Frursa na Vikwazo (O & OD iliyoboreshwa)
Aidha, katika makisio ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imejiwekea vipaumbele vyake pamoja na mikakati kumi na nne (14) itakayosaidia kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ili iweze kutekeleza Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 kwa asilimia 100
Makisio ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2022/2023
Akisoma taarifa kuhusu makisio ya mpango na bajeti ya mwaka 2022/2023 mbele ya Baraza la Madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Ndugu Jumanne Shauri, alisema "Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kukusanya Shilingi Bilioni 73.9 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani"
Matumizi ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2022/2023
"Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2022/2023 kwenye Mapato yake ya Ndani inatarajia kutumia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 73.9 katika mchanganuo ufuatao; Matumizi Mengineyo Shilingi Bilioni 22.04 sawa na 29.8% ya Bajeti, Mishahara Shilingi Bilioni 1.26 sawa na 1.7% ya Bajeti, Miradi ya Maendeleo Shilingi Bilioni 34.96 sawa na 47.26% ya Bajeti na Vyanzo Fungiwa Shilingi Bilioni 15.69 sawa na 21.21% ya Bajeti" Mkurugenzi Shauri
Makisio ya fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu
Ruzuku ya Shilingi Bilioni 119.9 kutoka Serikali Kuu imegawanywa katika maeneo mawili ambayo ni Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo
Mchanganuo wa Matumizi ya kawaida kwa fedha ya Ruzuku
"Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 98.15 ya fedha ya ruzuku sawa na 81.83% kulipa Mishahara na Shilingi Bilioni 2.628 sawa na 1.77% sawa na 1.47% kwa ajili ya Matumizi Mengineyo" alisema Shauri
Mchanganuo wa fedha za Miradi ya Maendeleo kwa fedha ya Ruzuku
Katika kipindi kijacho cha 2022/2023 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kutumia Shilingi Bilioni 19.99 kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambayo ni sawa na 16.66%.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.