BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo Tarehe 10 Februari, 2023limefanya Mkutano Maalum wa Mapitio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2022/2023 kwa kipindi cha nusu mwaka (Julai-Desemba, 2022) na kufanya Makadirio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2023/2024 wenye Jumla ya Shilingi Bilioni 218.2, ambapo kati ya fedha hizo kiasi cha Shilingi Bilioni 90.7 sawa na 41.56% ya Bajeti yote ni makusanyo kutoka vyanzo vya mapato ya ndani ya Halmashauri na Shilingi Bilioni 127.5 sawa na 58.43% ya Bajeti ni fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo ni kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya kawaida.
Aidha, kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou na kuongozwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mhe. Omary Kumbilamoto, kilipokea, kikajadili na kisha kupitisha Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 ambapo Bajeti ya Mapato ya ndani ya Halmashauri imeongezeka kwa 10.7% ukilinganisha na Bajeti ya Shilingi Bilioni 80 ya mwaka 2022/2023, hii imetokana na mikakati bora iliyowekwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwenye ukusanyaji wa mapato na uibuaji wa vyanzo vipya vya mapato. Katika Makadirio ya Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imeweka Mikakati Saba (07) itakayosaidia kufanikisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri ili iweze kutekeleza Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 kwa asilimia 100, pamoja na kuwa na Vipaumbele Kumi (10) vya Mpango na Bajeti.
Makadirio ya Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2023/2024
Akisoma taarifa kuhusu makadirio ya mpango na bajeti ya mwaka 2023/2024 mbele ya
Baraza la Madiwani, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Injinia Amani Mafuru alisema "Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kukusanya Shilingi Bilioni 90.7 kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani"
Matumizi ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kwa mwaka 2022/2023
"Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kwenye Mapato yake ya Ndani inatarajia kutumia fedha kiasi cha Shilingi Bilioni 90.7 katika mchanganuo ufuatao; Matumizi Mengineyo Shilingi Bilioni 20.5 sawa na 22.6% ya Bajeti, Miradi ya Maendeleo Shilingi Bilioni 47.9 sawa na 52.8% ya Bajeti na Vyanzo Fungiwa Shilingi Bilioni 22.3 sawa na 24.5% ya Bajeti" alisema Injinia Mafuru
Makadirio ya fedha za Ruzuku kutoka Serikali Kuu
Ruzuku ya Shilingi Bilioni 127.5 kutoka Serikali Kuu imegawanywa katika maeneo mawili ambayo ni Matumizi ya Kawaida na Miradi ya Maendeleo
Mchanganuo wa Matumizi ya kawaida kwa fedha ya Ruzuku
"Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam inatarajia kutumia Shilingi Bilioni 107.3 ya fedha ya ruzuku sawa na 84.1% kulipa Mishahara na Shilingi Bilioni 1.36 sawa na 1.06% kwa ajili ya Matumizi Mengineyo" alisema Injinia Mafuru
Mchanganuo wa fedha za Miradi ya Maendeleo kwa fedha ya Ruzuku
Katika kipindi kijacho cha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imepanga kutumia Shilingi Bilioni 18.6 kutekeleza Miradi ya Maendeleo ambayo ni sawa na 14.5%. Katika kuandaa Rasimu ya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam imezingatia Mwongozo wa uandaaji wa Bajeti uliotolewa na Hazina Mwezi Desemba 2022, Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 hadi 2025, Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoitoa Bungeni.
Sambamba na hayo, lakini pia uandaaji wa Rasimu ya Mpango na Bajeti umezingatia Sheria ya Bajeti Na. 11 ya mwaka 2015 sura 439 pamoja na kanuni zake, Mkakati wa Taifa wa Mapambano dhidi ya rushwa awamu ya Tatu, Malengo ya Maendeleo Endelevu, Mpango wa Mkakati wa Taifa wa kukuza uchumi na kupunguza umasikini Tanzania (MKUKUTA) II , Maoni ya wadau mbalimbali wa Halmashauri ambao wameshiriki katika maandalizi ya bajeti hii kuanzia ngazi ya Mtaa, Kata, Idara hadi Halmashauri kwa ujumla kwa kutumia mfumo wa Fursa na Vikwazo (O & OD iliyoboreshwa).
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.