Katika kutekeleza agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Angellah Kairuki wakati wa ziara yake alipotembelea Jimbo la Segerea katika shule ya Msingi Kifuru mnamo tarehe 1, Machi 2023 aliagiza Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kuhakikisha wanaleta madawati 500 kwa wanafunzi wa kifuru.
Hivyo Katika kutekeleza agizo hilo, leo Machi 09, 2023 Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kwa Kushirikiana na Mkurugenzi wa DCB Bank wameweza kukabidhi madawati 500 kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kifuru.
Akikabidhi Madawati hayo Mkurugenzi wa DCB Bank Ndg. Isdory Msaki ameeleza kuwa “Katika kutambua jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza na kuendeleza sekta ya Elimu Nchini sisi kama DCB tumekuja na kauli mbiu isemayo ‘Elimu Mpango Mzima na Mama’ ambayo inalenga kuhamasisha suala zima la elimu nchini kwa watoto wetu hivyo tuhakikishe tunatumia vyema fursa ya elimu bure na kuwapeleka watoto wetu shuleni kupata elimu bora.”
Sambamba na hilo Ndg. Msaki amewataka wanafunzi wa Shule ya Msingi Kifuru kusoma kwa bidii kwani jamii inatambua umuhimu wa elimu na ndiyo maana Bank ya DCB imeweza kuchangia madawati kwaajili ya kuwasaidia wanafunzi hao kusoma katika mazingira bora na salama.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Eng. Amani Mafuru amesema “Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa Bank ya DCB kwani Waziri wa OR-TAMISEMI alipotoa maagizo ya kuleta madawati katika Shule hii tuliongea na Mkurugenzi wa DCB na yeye kama mdau wetu aliweza kutusaidia madawati 30 ambayo leo hii tumeweza kukabidhiwa hivyo nipende kusema yote tuliyoagizwa na Mheshimiwa Waziri kuyatekeleza tutayatekeleza ipasavyo hatua kwa hatua na tumeanza na hili.”
Sambamba na hilo Eng.Mafuru amewataka wanafunzi kusoma kwa bidii kwani hayo yote yanatekelezwa ili kuwajengea wao mazingira rafiki ya kusoma na kupata elimu bora.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wanafunzi wengine Dada Mkuu wa Shule ya Msingi Kifuru Sarah Edwine amesema “Namshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea madarasa, pia napenda kumshukuru Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na Mkurugenzi wa Bank ya DCB kwa kutekeleza agizo la Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Kairuki na kutuletea madawati kama walivyoagizwa hivyo niwaahidi tutasoma kwa bidii na tutafaulu kwa kiwango cha juu zaidi kama mlivyotutekelezea hili na sisi tunaenda kuongeza ufaulu katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa Shule za Msingi.”
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.