Na: Doina Mwambagi
Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), chini ya Mwenyekiti wake Dr. Alhad Mussa Salum Leo tarehe 22 mei 2025, imefanya ziara ya kutembelea soko la kisasa la nyama choma la Kumbilamoto lililopo Vingunguti, kwa lengo la kujionea maendeleo ya mradi huo na kutambua mafanikio ya serikali katika kuboresha maisha ya wananchi.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa JMAT, Dr. Alhad amesema
“Tunashukuru kualikwa kutembelea mradi huu wa kimkakati na wa kombozi kwa wananchi. Maendeleo tuliyoyaona hapa yametufurahisha sana. Tumeridhika kuona kuwa wananchi wameondokana na adha walizokuwa wakizipata wakati wa jua kali na mvua. Tunatoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuweka mazingira bora ya kazi kwa watu wa kipato cha chini.”
Aidha, JMAT imesisitiza kuwa kusaidia kazi za mikono kwa wananchi ni njia madhubuti ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja, huku ikitoa wito kwa watanzania kuendeleza mshikamano na kumuomba Mungu aendelee kuilinda nchi kwa amani na utulivu ili kazi iendelee kufanyika kwa mafanikio.
Katika ziara hiyo, Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Omary Kumbilamoto, ametoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya masoko huku akimpongeza Mkurugenzi wa Jiji hili Ndugu Elihuruma Mabelya, kwa kusimamia na kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa viwango vya kisasa.
Soko hilo la kisasa linategemea kuwa na zaidi ya wafanyabiashara 232, wakiwemo wauzaji wa nyama choma, mama lishe, wauzaji wa vinywaji, mbogamboga na viungo. Soko hilo linatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa wastani wa shilingi milioni 11 kila mwezi, ambayo ni zaidi ya shilingi milioni 100 kwa mwaka. Ujenzi wa soko hili umegharimu kiasi cha shilingi milioni 700.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.