Na: Hashim Jumbe
Kamati ya Fedha na Utawala Halmashauri ya Jiji la DSM, leo tarehe 04 Mei, 2021 imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri hiyo kwa kipindi cha robo ya Tatu (3) ya kuanzia Januari hadi Machi, 2021, Kamati hiyo ambayo moja kati ya majukumu yake ni kuhakikisha Miradi yote ya Maendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri inapata usimamizi wa kutosha ikiwa pamoja na kupima thamani halisi ya fedha zinazotumika kwenye Miradi hiyo.
Aidha, ziara hiyo ni ya kawaida na inatoa fursa kwa wajumbe wa Kamati hiyo kuweza kukagua na kutolea mapendekezo Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa na Halmashauri kwa kipindi husika.
"Leo tumefanya ziara na kamati ya fedha, lengo na madhumuni ni kukagua miradi yote ya kimkakati ambayo sisi tunaisimamia kama Jiji, na miradi hii ya kimkakati ni mwendelezo wa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo iliahidi kwa Wananchi, tumeanzia kwenye machinjio ya vingunguti ambapo kule mradi umegharimu takribani Bilioni 12.48 na hatua iliyobaki ni kuweka zege nje" alisema Mhe. Omary Kumbilamoto, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam
Lakini pia kamati ya fedha na utawala ilitembelea na mradi wa pili wa kimkakati ambao ni Ujenzi wa Soko la Kisutu, ambapo Mstahiki Meya Kumbilamoto alieleza "tumekuja kutembelea ujenzi wa mradi wa Soko la Kisutu, mradi huu una thamani ya takribani Bilioni 13.49 na teyari mradi umefikia 97% kinachosubiriwa hapa ni 'lift' na tunatumaini wafanyabiashara mwishoni mwa mwezi huu wanaweza kuingia"
Mhe. Kumbilamoto aliendelea kueleza kuwa "mwanzo tuliwakuta wafanyabiashara 669, lakini niwashukuru Serikali Kuu na Waheshimiwa Madiwani, hivi sasa Soko hili litabeba wafanyabiashara zaidi ya 1,500 maana yake tutaongeza mapato makubwa sana kwa Jiji letu la DSM na kutatua kero nyengine ambazo wananchi zinawakabili"
Itakumbukwa kuwa Kamati ya Fedha na Utawala ina jukumu la kusimamia miradi yote ya Halmashauri katika sekta ya elimu, afya, maji, kilimo, ufugaji pamoja na kuhakikisha 10% ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu inatolewa na Halmashauri kwa walengwa
Ziara hiyo itafuatiwa na kikao cha kamati kitakachojadili taarifa za utendaji kazi kwa idara na vitengo wanavyovisimamia pamoja na kupitia na kujadili taarifa ya miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2021
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.