Kamati ya Kudhibiti UKIMWI ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, leo tarehe 14 Agosti, 2024 wamefanya ziara ya kutembelea na kukagua shughuli zinazofanywa na Nacopha konga, yenye lengo la kuhamasisha jamii kwa kusaidia na kuwajengea uwezo watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI (WAVIU) ili waweze kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha.
Akiongea wakati wa ziara hiyo kwa niaba ya Mwenyekiti, Mhe. Lucy Lugome amesema “Nipende kuwashukuru sana kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kusaidia jamii ya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI hadi kutupelekea Leo hii kuja kukagua miradi yenu japo ni sehemu ya majukumu yetu lakini pia kutambua mchango wenu katika kutoa Elimu kwa Umma juu ya kudhibiti maambukizi mapya ya VVU na UKIMWI, hivyo ziara hii ni sehemu ya utekelezaji wa miradi pamoja na kuhakikisha huduma zote zinazotolewa kwa WAVIU zinatekelezwa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam”
Aidha, Mhe. Lugome ameongeza kuwa "Napenda kuwatia moyo, msikate tamaa kwasababu kuwa na maambukizi ya UKIMWI sio mwisho wa maisha , maisha lazima yaendelee hivyo kupitia vikundi vyenu vya maendeleo mfanye kazi kwa bidii Ili kujipatia vipato, pia kamati hii ni kamati ya vitendo nawaahidi mwaka huu wa fedha kupitia Halmshauri yetu tutahakikisha kila kikundi kinapata fedha kwa ajili ya kujiendeleza mfikie malengo mliyojipangia."
Awali akisoma taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Shirika kwa kipindi cha Machi – Juni 2024, Katibu wa Taasisi hiyo Bw. Boniface Kazinduki ameeleza kuwa kongwa ni mabaraza ya watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI ngazi ya Halmashauri yenye lengo la kuwaleta waviu pamoja ili kupata Elimu
Sambamba na hilo Bw kazinduki amesema “Konga inashughulika na kutoa elimu juu ya umuhimu wa matumizi sahihi ya dawa ARVs kwa waishio na maambukizi ya virusi vya Ukimwi (WAVIU) , hivyo naomba tupewe nafasi katika vituo vya afya kwa ajili ya kutoa Elimu na kutafiti watoro na hii itafanya konga iwe haikuliko kusubiri wadau mbalimbali wanapotokea”
Aidha, Kamati imeagiza Idara ya Afya kupeleka huduma za kiafya (mobile clinic) eneo la Pugu Mnadani ikiwa ni pamoja na huduma ya upimaji wa VVU , utoaji wa dawa pamoja na utoaji wa Elimu kuhusiana na VVU.
1 BARABARA YA MOROGORO 11882 DAR ES SALAAM
Postal Address: S.L.P 20950
Telephone: 0738 378 386
Mobile: 0738 378 386
Email: info@dcc.go.tz
Copyright © 2017 Dar es Salaam City Council . All rights reserved.